MANARA ANAVYOGOMBANA NA MANARA MWENYEWE

    “HAIWEZEKANI mpira ukaendeshwa kwa kulalamika lalamika, haiwezekani, niwapongeze sana TFF, Bodi ya Ligi na Serikali kwa kusimamia nidhamu ya mpira wa miguu ndani na nje ya uwanja wanatoa sapoti ligi inachezwa…..”

    Hizo ni baadhi ya kauli za msemaji wa mabingwa wa kihistoria Yanga SC, Haji Manara kipindi akiwa Simba ambapo alionyesha kuchukizwa waziwazi na kitendo cha baadhi ya viongozi wa Yanga na wazee wa Yanga kuilalamikia TFF na Bodi ya Ligi kuwa wanaipendelea Simba jambo ambalo lilipelekea aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kufungiwa miaka mitano kujihusisha na mchezo wa soka kabla ya kuomba radhi na adhabu yake kutenguliwa na Bodi ya Ligi kupitia Sekretarieti ya maadili.

    Kwenye dunia ya kisasa kuna mambo mawili ya kuogopa kuliko kitu chochote, mosi ni Mungu na jambo la pili la kuliogopa ni teknolojia, awali kabla ya kamati ya nidhamu kumkuta na hatia Manara baada ya kuonekana akizozana na Rais wa TFF Wallace Karia. Kabla ya hukumu Manara alitoka hadharani na kumuomba radhi Rais Karia pamoja na umma wa wapenda soka akionyesha kujutia kile alichokifanya huku akisisitiza kuwa kuomba kwake radhi kusizuie hukumu itakayotolewa na Sekretarieti ya maadili.

    Baada ya hukumu kutoka Haji Manara amekuja kwenye sura nyingine ambapo amefunguka shutuma nyingi dhidi ya Rais Karia jambo ambalo linaongeza mkanganyiko kwa wanafamilia wa soka nchini wanashindwa kumuweka kwenye engo ipi, teknolojia inaendelea kuwagombanisha Manara dhidi ya Manara.

    Manara anaendelea kukinzana na kauli zake mwenyewe kwani awali alijitokeza hadharani na kukiri lakini ghafla amerudi tena kwa sura nyingine.

    Suala hili amejaribu kutengeneza ajenda kuwa Yanga inaonewa lakini uhalisia wa mambo ni kwamba Yanga haihusiki kwenye kesi hii, hii ni ya Manara mwenyewe ambaye alipelekwa kamati ya maadili na si Yanga ambao wamepelekwa huko, hii imepelekea baadhi ya mashabiki na wanachama wa Yanga kuingia kichwa kichwa kwenye sakata hili bila kuchambua uhalisia wa kesi yenyewe.

    Manara si wa kwanza kufungiwa kujihusisha na soka wapo wengi ambao walikutwa na hatia na wakafungiwa linapokuja suala la kanuni haziangalii kama unatoka Simba, Yanga au Namungo kanuni zitafuata mkondo na kama utaona hujaridhishwa kuna nafasi ya kukata rufaa.

    Kipindi anaondoka Simba aliongea mambo mengi kuhusu viongozi wake wa zamani akiwashutumu kwa mambo mbalimbali, juzi pia kawaita waandishi na kuanza kulizungumzia upya sakata lake na Rais Karia hivyo ishu hii inawaweka njia panda hata wale ambao walikuwa wanahisi Manara kaonewa kwani wanashindwa washike lipi na waache lipi.

    Manara anachopaswa kufanya ni kutulia na kuchukua maamuzi sahihi kama kukata rufaa akumbuke kuwa teknolojia kamwe haijawahi kuwa nyuma.

    Previous articleSAUTI:ZIJUE NAMBA AMBAZO WATAVAA MASTAA WA YANGA
    Next articleSIMBA WAIVUTIA KASI YANGA NGAO YA JAMII