SIMBA WATAJA SABABU YA KUMPA DILI KIUNGO MZAMIRU

UONGOZI wa Simba umesema sababu ya kumuongeza mkataba Mzamiru Yassin ni uwezo wake jambo ambalo limewafanya waweze kukaa naye mezani na kumpa dili jipya.

Mzawa huyo mwenye uwezo wa kupanda na kushuka alikuwa na nafasi kikosi cha kwanza msimu wa 2021/22 kwenye mechi za ligi na zile za kimataifa.

Ni dili la miaka miwili ameongeza rasmi  na atakuwa  mpaka 2024 akiwa kwenye uzi mwekundu.

Ahmed Ally,Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa moja ya sababu za kumuongezea mkataba kiungo huyo ni uwezo wake.

“Hakuna ambaye ana mashaka na uwezo wa Mzamiru na ni moja ya wachezaji waliodumu kwa muda mrefu ndani ya Simba ikiwa ni pamoja na Jonas Mkude ambaye huyu yupo kwa muda mrefu.

“Uwezo wake upo wazi na hii ni sababu ya kuweza kumuongezea mkataba ndani ya Simba tuna amini kwamba ataendelea kuwa pamoja nasi kwa ajili ya kutimiza majukumu,” amesema.

Mzamiru kwa sasa yupo kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania,Taifa Stars ambayo inajiandaa kucheza mechi za kuwania kufuzu CHAN dhidi ya Somalia.