UPEPO WA USAJILI UNAHITAJI UMAKINI MKUBWA

IKIWA umetulia kwa sasa na kutazama upepo ambavyo upo lazima utasikia kuhusu namna ambavyo kila mwenye nguvu anaingia sokoni kusaka kile ambacho anakihitaji.

Huu ni upepo mzuri hasa kwa kila mmoja kupata kile ambacho anakitaka muda huu wa kufanya maandalizi ya usajili kwa wachezaji ambao wanahitajika.

Wapo wachezaji ambao wameshapewa mkono wa kwa heri mapema kwa timu zilizofanya hivyo zinastahili pongezi kwa kuwa zamani timu zilikuwa zinawaacha wachezaji muda mfupi kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Unapozungumzia mchezaji maisha yake yeye ni mpira na anahitaji kufanya maisha kupitia mpira inapotokea ukashindwa kumpa taarifa mapema utakuwa umezuia mambo yake kuendelea.

Ukweli ni kwamba wapo ambao huwa wanapenda kufich taarifa zinazowahusu wachezaji kwa kile ambacho wanakuwa wakiamini kwamba wanamuweka mchezaji sokoni.

Hilo halipo kwa sasa na kwa timu ambazo zinafanya hivyo zinatakiwa kubadilika na kuongeza nguvu kwenye suala la uwekezaji wachezaji wazuri na kutoa taarifa kwa haraka zaidi.

Namna ambavyo mwendo wa ligi umekwenda na sasa ni muda wakufanya usajili na maandalizi ya msimu ujao kwa kuwa msimu wa 2021/22 umegota ukingoni.

Hapa mwendo wa kutazama ile ripoti ya makocha ambayo imetolewa hivyo ni muhimu kuanza kuifanyia kazi mapema.

Ukizingatia kwamba ratiba ya ligi imeshatolewa hasa kwa mechi za mwanzo pamoja na ile ya Ngao ya Jamii nah ii inamaanisha kwamba Agosti mambo yanarejea upya.

Kwa timu ambazo zimeshuka daraja ni muda wao kufanya maandalizi kwa ajili ya wakati ujao kwa kuwa nafasi ipo.

Kama waliweza kupanda sasa wameweza kushuka na wana nafasi nyingine ya kuweza kurejea kwenye ligi kwa msimu ujao ikiwa mipango itakweda kwa umakini.

Ambazo zimepanda pongezi kwa mara nyingine tena lakini wanapaswa kuelewa kwamba maisha ya kwenye ligi ushindani ni kila siku.

Ikiwa watakuja na hesabu ambazo wametoka nazo kule ndani ya Championship wanaweza kukwama kwa kuwa mbinu huku ni tofauti kabisa.

Hivyo ambacho wanatakiwa kufanya ni kuwa na wachezaji wenye uzoefu,benchi lenye uwezo wa kusoma mchezo na kubadili mbinu haraka zaidi.

Pia zile ambazo zinacheza hatua ya mtoano nazo zina kazi ya kuwapa matokeo mazuri wale mashabiki wao hasa kwa kushinda mechi zao kwani ili ushinde lazima ufanye maandalizi ya kushinda.

Ikiwa maandalizi yatakuwa ni hafifu leo maana yake ni kwamba kesho hakutakuwa na matokeo mazuri kwa timu ambazo zitacheza kusaka ushindi.

Kwa upande wa mashabiki ambao wanajitokeza kwenye mechi ni muda wa kuwa makini na kuacha masuala ya ugomvi,maisha ya mpira ni amani na upendo.

Kwa wale ambao wanapenda ugomvi hao wanapaswa watulie wakiwa nyumbani kutazama namna maisha ya mpira yanavyokwenda.

Imeandikwa na Dizo Click.