Aliyekuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Hitimana Thierry, amevunja ukimya na kutaja kuwa kukamiwa na kuchezewa kwa nguvu nyingi na wapinzani wao ndiyo chanzo kikubwa cha wao kupata kadi nyekundu kwenye mechi wanazocheza nao.
Hitamana ametoa kauli hiyo kufuatia kutokea kwa kadi nne nyekundu walizopewa wapinzani wao katika mechi nne kati ya tano walizocheza mpaka sasa kwenye ligi kuu.
Katika mchezo wa pili dhidi ya Dodoma Jiji, ilitoka kadi nyekundu ya kwanza kabla ya kadi ya pili kutolewa katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania, kisha katika mchezo wa Coastal Unioni na mwisho ukiwa wa Namungo.
Hitamana alisema kuwa moja ya jambo gumu ambalo wamekuwa wakikutana nalo tangu kuanza kwa msimu huu ni wachezaji wao kucheza kwa kukamiwa na wapinzani wakiwa na lengo la kuwaumiza jambo ambalo limekuwa likiwarudisha nyuma katika kupata matokeo.
“Unajua kumekuwa na mambo mengi sana ambayo yanaendelea katika mechi zetu lakini kubwa tumekuwa tukikamiwa katika kila mchezo kwa wapinzani kucheza soka la nguvu ambalo limepelekea kuwa na kadi nyingi nyekundu kwenye mechi zetu.
“Kiukweli inaumiza kwa sababu inaonyesha hii ni dhamira ya makusudi ambayo inatukwamisha wakati mwingine kwa sababu siyo kitu rahisi kuwakosa wachezaji muhimu kwenye mechi zetu, nadhani ni wakati wa timu kucheza mpira siyo kukamiana,” alisema.