MCAMEROON KUCHUKUA MIKOBA YA LWANGA SIMBA

WAKATI wakijua kuwa wataachana na kiungo wao mkabaji, Taddeo Lwanga, uongozi wa Simba upo kwenye mawindo makali ya kumchukua kiungo Cedric Zemba Ekong raia wa Cameroon ili azibe pengo hilo.

Simba wanataka kuliboresha eneo lao la ukabaji ambapo Ekong anayeitumikia Apejes FC ya kwao akifanywa kuwa chaguo namba moja.

Kikosi hicho kwa msimu huu kimekuwa na tatizo kwenye eneo hilo kutokana na nyota wake Sadio Kanoute na Jonas Mkude muda mwingi kuandamwa na majeraha.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo Championi Jumamosi limezinasa ni kuwa, Ekong ni moja ya wachezaji ambao majina yao yapo kwenye listi maalum ya usajili wa timu hiyo.

“Ekong ni mmoja kati ya wachezaji ambao wanahitajika ndani ya Simba, ni kiungo mzoefu kidogo kulingana na timu ambazo amezicheza.

“Mazungumzo yanakwenda vizuri na usishangae kuona muda wowote mchezaji huyo akawa ni mali yetu, tunaamini kila kitu kitaenda sawa,” kilisema chanzo hiko.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habri wa Simba, Ahmed Ally alithitbitisha Simba kuingia sokoni na kwa kuendelea kufanya usajili wa wachezaji wengi wa kimataifa bila ya kuyataja majina yao.

“Ni ngumu kuweka wazi wachezaji gani wataingia ndani ya Simba na wale watakoachwa na taarifa tu kwa Wanasimba wanatakiwa kufahamu kuwa tutafanya usajili wa wachezaji wengi wa maana kutoka nje ya nchi lakini lazima wengine wapungue kama ambavyo mipango ya timu imejiwekea,” alisema kiongozi huyo