MENEJA wa wachezaji wa Yanga, Djuma Shabani na Yanick Bangala, anayefahamika kwa jina la Faustino Mukandila, tayari ameshatua jijini Dar kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa timu hiyo ili kuongezewa mikataba kwa nyota wake hao wawili.
Djuma Shabani na Bangala wote wamekuwa tegemeo ndani ya Yanga msimu huu ambapo wamefanikiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Yanga na kuifanikisha timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara baada ya kuukosa kwa misimu minne.
Akizungmza na Championi Jumatatu, Faustino ambaye ni meneja, alisema kuwa: “Djuma na Bangala wote walisaini mikataba ya miaka 2 kuitumikia Yanga mwaka jana mwezi wa sita ambapo kwa sasa wamesalia mwaka mmoja pekee katika mikataba yao, jambo ambalo ni lazima kufanyike majadiliano mapya ya kuongezewa mikataba mipya.
“Hivyo, ndio maana nimekuja nchini kwa ajili ya kazi hiyo huku nikiamini kila kitu kitakwenda sawa kulingana na ubora wa wachezaji wangu ambao wameuonyesha ndani ya Yanga na mchango wao kuwa mkubwa na ulioipa mafanikio makubwa Yanga msimu huu,” alisema kiongozi huyo.