MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Kalala Mayele, amesema kuwa baada ya kumaliza zoezi lake la kwanza la kuipa ubingwa timu hiyo, kwa sasa anatafuta zoezi lake la pili la kuhakikisha kuwa anakuwa mfungaji bora mbele ya George Mpole wa Geita Gold ambaye wanafukuzana naye.
Mayele na Mpole wote kwa sasa wamelingana katika kugombea tuzo ya ufungaji bora wote wakiwa na mabao 16 huku wakiwa wamebakiza michezo mitatu ya mwisho.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mayele alisema kuwa jambo zito katika akili yake lilikuwa ni la kuhakikisha kuwa anaipatia Yanga ubingwa na kwa kuwa tayari amefanikiwa, kwa sasa anatafuta jambo la pili ambalo ni kuhakikisha anaibuka na tuzo ya mfungaji bora wa ligi kuu msimu huu mbele ya Mpole.
“Ndio, ni kweli Mpole anafanya vizuri na ukiangalia tunakimbizana vizuri lakini lazima nipambane kwa kila namna kuhakikisha nafanikiwa kuwa mfungaji bora msimu huu.
“Ukiangalia deni kubwa ambalo nilikuwa nalo msimu huu ni kuhakikisha naifanikisha Yanga inakuwa bingwa kama ambavyo niliahidi na namshukuru Mungu hilo limekamilika na kwa sasa kilichobaki ni mimi kupambana ili nifunge mabao mengi na kuibuka kinara wa ufungaji,” alisema Mayele.