SIMON MSUVA ATAJWA KUINGIA RADA ZA YANGA

IMEELEZWA kuwa nyota wa zamani wa kikosi cha Yanga, Simon Msuva yupo kwenye hesabu za mabosi wa Yanga ambao wanahitaji kumuongeza ndani ya kikosi hicho.

Msuva ni winga wa kimataifa ambaye yupo Tanzania kwa sasa baada ya kuweza kutokwenda sawa na mabosi wake Wydad Casablanca ya Morocco na suala lao lipo Fifa.

Nyota huyo amekuwa akipewa nafasi kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars na anacheza kwenye mechi za kirafiki akiwa na kituo cha Cambiasso.

Habari zinaeleza kuwa Msuva ni miongoni mwa mastaa ambao wanakubalika Yanga hivyo anaweza kurejea kwa mara nyingine.

“Msuva ni mchezaji mzuri na anaweza kurejea Yanga kwa kuwa alicheza kwa mafanikio hapo,ikiwa utaratibu utakuwa sawa anaweza kujiunga na Yanga,” ilieleza taarifa hiyo,”.

Haji Manara, Ofisa Habari wa Yanga hivi karibuni alisema kuwa watafanya usajili makini kwa ajili ya kufanya vizuri kimataifa.

Yanga ni mabingwa wa ligi baada ya kucheza mechi 27 wamekusanya pointi 67 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine na bado wana mechi tatu mkononi kukamilisha mzunguko wa pili.

Msuva alikuwa kwenye kikosi cha Yanga cha msimu wa 2016/17 na ilikuwa ni mara ya 27 kutwaa ubingwa kwa Yanga.