KAMA ulikuwa huamini, basi taarifa ikufikie kwamba, Yanga imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Stephane Aziz Ki na siku ya kutua nchini imetajwa.
Ipo hivi, mchezaji huyo kwa taarifa za uhakika ambazo imezipata Spoti Xtra, ataingia nchini mapema ndani ya wiki ambayo inaanza kesho Jumatatu kwa ajili ya kumalizana kila kitu na Yanga.
Baada ya kumalizana katika masuala ya kusaini mikataba, atangazwa ndani ya mwezi huu, yaani hadi kufikia Juni 29, kila kitu kitakuwa wazi juu ya usajili wake.
Mtoa taarifa huyo alisema, mara baada ya Aziz Ki kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu huu akiwa na ASEC hivi karibuni, ataingia nchini kwa ajili ya maandalizi hayo ya kutambulishwa ikiwemo kutengenezewa video pamoja na kupigwa picha kama ilivyotokea kwa Lazarous Kambole.
“Unajua Aziz Ki mkataba wake unamalizika Juni 28, mwaka huu, hivyo Yanga kwa sasa haiwezi kumtambuisha kama ni mchezaji wao halali.
“Ambacho kitafanyika wiki inayoanzia Jumatatu, Azizi Ki atatua nchini kisha atamalizana na Yanga na mambo ya picha pamoja na video za utambulisho zitafanyika, baada ya hapo watasubiri mpaka ipite tarehe 28 kisha watamtangaza kuanzia tarehe 29. Utambulisho wake utakuwa wa kipekee, kama mfalme.
“Lakini pia inawezekana pia wakamtangaza kabla ya tarehe hizo kama tu Yanga watakuwa wamezungumza vizuri na viongozi wa ASEC na kupewa ruhusa ya kufanya hivyo.
Hivi karibuni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said, alisema: “Yanga ikimuhitaji mchezaji yeyote haiwezi kumkosa, hivyo kama tunamuhitaji Aziz Ki, basi lazima tumpate.”