Home Sports SIMBA YAMALIZANA NA BEKI KATILI KUTOKA BURUNDI

SIMBA YAMALIZANA NA BEKI KATILI KUTOKA BURUNDI

INAELEZWA mabosi wa Simba wamepania kufanya makubwa msimu ujao kufuatia kumnasa beki wa zamani wa Chipa United, Mrundi, Frédéric Nsabiyumva.

Beki huyo wa kati mwenye miaka 27, amekuwa akisifika nchini Burundi kama mmoja kati ya mabeki wa kati makatili kutokana na uwezo mkubwa alionao wa kukaba washambuliaji wasumbufu.

Usajili wa beki huyo unatajwa ni sehemu ya Simba kuimarisha kikosi chao kiweze kupambana na wapinzani wao msimu ujao wakiwemo Yanga ambao hivi karibuni walimtambulisha rasmi mshambuliaji Lazarous Kambole kuwa ni usajili wao wa kwanza.

Nsabiyumva na Kambole wote wanakuja kucheza Ligi Kuu Tanzania wakitokea Afrika Kusini. Kambole raia wa Zambia ametokea Kaizer Chiefs.

Mrundi huyo hivi karibuni alikuwepo hapa nchini na timu ya taifa ya Burundi ambayo ilitumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2023 dhidi ya Cameroon.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kimeliambia Spoti Xtra kwamba, viongozi wa timu hiyo wamekamilisha mazungumzo na beki huyo kwa kufikia makubaliano ya kuingia mkataba wa miaka miwili.

“Frédéric amefanya mazungumzo na mabosi wa Simba hapahapa Dar es Salaam wakati alipokuwa na timu ya taifa katika siku chache zilizopita ambapo alikuwepo na timu yake ya taifa.

“Kikubwa walimekubaliana mkataba wa miaka miwili, lakini bado kuna vitu vilikuwa havijakaa sawa, mchezaji aliomba muda kidogo akitaka mpaka arudi Afrika Kusini yalipo makazi yake, kisha ndipo wakamilishe dili hilo,” alisema mtoa taarifa.

Spoti Xtra halikuishia hapo, lilimtafuta mmoja kati ya wachezaji wa timu ya taifa Burundi ambaye alikuwepo jijini Dar na kikosi hicho, alisema kuwa uwezekano mkubwa wa beki huyo kujiunga na Simba kwa kuwa alikutana na viongozi wa timu hiyo wakiwa hotelini.

“Hilo suala siyo geni maana hata mwenyewe alikuwa anatuambia anatamani kucheza ligi ya Tanznaia kwa sababu sasa hivi ana timu yoyote japokuwa yupo Afrika Kusini na amekuwa akifanya mazoezi na timu ya Jomo Cosmo ambayo ipo chini ya Jono Somo ambaye ndiye meneja wake,” alisema mchezaji huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia usajili wa timu yao akisema: “Mashabiki wa timu yetu watulie, uongozi unaendelea kushusha vifaa vipya, tutaendelea kuweka wazi kadiri muda unavyokwenda.”

Previous articleYANGA YATAJA SIKU YA AZIZ KI KUTUA
Next articleAZIZ KI, MORRISON WAIPA JEURI YANGA