KINARA wa mabao wa Ligi Kuu Bara, Mkongomani Fiston Mayele ameibuka na kumwambia mpinzani wake wa Geita Gold, George Mpole hatakubali akiache kiatu cha ufungaji bora msimu huu.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kufunga mabao mawili na kufikisha mabao 16 katika ufungaji huku mpinzani wake akifunga 15.
Mkongomani huyo alifunga mabao hayo katika mchezo wa ligi waliocheza dhidi ya Coastal Union ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar na kumalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-0.
Mayele amesema kuwa anaheshimu kiwango bora cha Mpole ambacho kinamfanya yeye aongeze juhudi ya kuendelea kufunga.
Mayele amesema kuwa licha ya kiwango bora alichonacho Mpole, hamhofii na badala yake ataendelea kupambana uwanjani ili kuhakikisha anamzidi kwa mabao.
“Mimi na Mpole kila mmoja anaipambania timu yake ipate ushindi kwa kutumia vema kila nafasi anayoipata katika kufunga mabao.
“Awali kasi yangu ya kufunga mabao ilipungua kutokana na presha iliyokuwepo ya ubingwa, lakini baada ya kujihakikishia nafasi ya ubingwa wa ligi, nitacheza kwa utulivu ili kufanikisha malengo yetu.
“Haikuwa rahisi kwangu kuchukua ubingwa, bila ya kupambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu kufanikisha malengo yetu,” amesema Mayele.