YANGA YATWAA UBINGWA WA 28 BONGO

YANGA imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa ambapo timu zote zilikuwa zinahitaji kupata ushindi.

Dakika 15 za mwanzo Coastal Union ilianza kwa kasi ila mipango ilikuwa inakwama kwenye miguu ya Dickson Job na Yanick Bangala ambao walikuwa mabeki wa kati.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Fiston Mayele ambaye alitupia mabao mawili na kufanya awe amefunga mabao 16 huku bao moja likifungwa na Chico Ushindi.

Yanga inatwaa ubingwa mbele ya Coastal Union ikiwa imebakiza mechi tatu mkononi kukamilisha mzunguko wa pili.

Ni pointi 67 inazo kwa sasa ambazo hazitafikiwa na timu yoyote ndani ya Bongo kwa msimu wa 2021/22.

Unakuwa ni ubingwa wa 28 kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi na msaidizi wake ni Cedrick Kaze.