BAADA ya tetesi nyingi kuzagaa za kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Luis Miquissone raia wa Msumbiji kurejea katika timu hiyo, uongozi wa Simba SC umeibuka na kufungukia ishu nzima.
Luis alijiunga na Al Ahly Agosti 26, 2021 kwa mkataba wa miaka minne akitokea Simba baada ya kucheza kwa takribani msimu mmoja na nusu kuanzia Januari 3, 2020. Mkataba wake utaisha 2025.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi, amesema kuwa, kwa sasa ni ngumu Al Ahly kumtoa kiungo huyo na kurudi Simba.
Nghambi amesema ugumu huo unatokana na kiungo huyo kuwepo katika mipango ya benchi la ufundi la timu yake hiyo.
“Ngumu kwa sasa kumpata mchezaji anayecheza timu kubwa zilizopo katika Ukanda wa Afrika, hapo nazuzungumzia Al Ahly, Zamalek, Wydad Casablanca, Kaizer Chiefs na nyinginezo.
“Hivi sasa Luis ameanza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo ngumu kumpata kirahisi kama watu wanavyofikiria.
“Labda itokee lakini hadi hivi sasa bado hatujapata taarifa rasmi za kiofisi kutoka Al Ahly juu ya Luis kutolewa kwa mkopo,” amesema Nghambi.
Kiungo huyo hivi karibuni tetesi nyingi zilimuhusisha kuwa njiani kurejea Simba kwa kile kilichoelezwa klabu yake kupanga kumtoa kwa mkopo baada ya msimu huu kumalizika.