MPAKA sasa majina ambayo yanatajwa huenda wanahusika kusajiliwa ndani ya Liverpool ni Darwin Nunez, Christopher Nkunku, Jude Bellingham, Pablo Gavi, Cristopher Ramsey na wengine wengi.
Hii imekuwa kawaida kwa timu kubwa barani Ulaya na bora kama Liverpool kutopoa katika masuala ya usajili haswa katika kipindi kama hiki.
Nguvu ya ushawishi tunayo, mafanikio makubwa Ulaya tunayo, wachezaji wazuri na bora Ulaya pia tunao, hivyo wachezaji wengi wanatamani kucheza kwenye timu yetu.
Inawezekana ikawa ni ngumu kwa watu kuamini haya mambo, lakini amini kuwa msimu huu Liverpool itatumia pesa nyingi sana katika usajili tofauti na vipindi vingine vyote.
Unakumbuka mara ya mwisho Liverpool kutumia pesa nyingi basi iliwasajili Allison Becker, Virgil Van Dijk na Fabinho Tavares basi na msimu huu tarajia kuona Liverpool tukifanya hivyo.
Pengine akili ya kawaida ipo hivi, baada ya Liverpool kushindwa kubeba mataji makubwa mawili yaani EPL na UEFA, mabosi wa Liverpool kuna kitu wamegundua haswa ndani ya timu.
Katika eneo la ushambuliaji timu imekosa mshambuliaji wa maana yaani straika wa kati jambo ambalo nafasi nyingi za kufunga mabao zinakoswa pale mbele.
Hapo sasa ndipo unapoona Nunez anahitajika, pili wakaona hakuna kiungo wa maana mwenye uwezo wa kufunga mabao ya kutosha jambo ambalo wanahitaji kuboresha, tayari Fábio Carvalho amesajiliwa na sasa wanaangaliwa wengine.
Mabosi pia wakitazama kwa majirani yaani Manchester City wanaona kuwa wamemsajili Erling Haland jambo ambalo ni lazima tuende nao ngadu kwa ngadu na sasa ameletwa Nunez.
Katika hayo yote napata picha ya jinsi gani Liverpool tutaenda kutisha msimu ujao..?
Utatu wetu mtakatifu msimu ujao utakuwa hivi msiogope jamani, Diaz atakuwa kushoto halafu kulia atakuwepo Mohammed Salah kisha katikati atakuwepo jibaba lenye miraba sita, Darwin Nunez.
Julian Wards ambaye ni Sporting Director mpya wa Liverpool ndani ya wiki moja ofisini ameonesha pasipo na shaka kwamba viatu vya mtangulizi wake Michael Edward ni saizi yake kabisa.
Pauni milioni 80 ameipeleka tayari kwa watoto wa Eusebio pale Benfica na dili la kumnasa Nunez liko jirani na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kuwa mchezaji wa Liverpool .
Lakini wakati Nunez akiwa anajiandaa kuja Liverpool, Ward ndani ya wiki hiihii amekataa ofa kutoka kwa Bayern Munich ya kumnasa Sadio Mane.
Nunez anatarajiwa kutua ndani ya wiki hii, halafu dili ambalo linafuata kwa upande wetu litatupwa huko Ujerumani kwenda kumrudisha mwana wa Malkia, kipenzi cha Buckingham Palace, Golden Boy Jude Bellingham.
Kisha anafuata Jarrod Bowen, Nkuku ama Raphinha na wengine wengi.
Klopp alivyosema tu-book hoteli pale Istanbul msimu ujao kwenye fainali ya UEFA hakuwa anatania. Alikuwa siriaz. Twenzetuni.
Nawakumbusha Uruguay hawajawahi kuwa na straika mbovu, tukianzia kwa Diego Forlan, Luis Suarez, Edinson Cavan na sasa ni zamu ya Darwin Nunez, kwa bahati nzuri Suarez amewahi kucheza Liverpool, hivyo atamueleza kila kitu Nunez.
Kwa ambao hawajawahi kumuona Nunez anavyocheza basi wakifikiria yule Fernando Torres wa Liverpool basi watapata picha halisi ya Nunez.