TEN HAG NA MTEGO WA USAJILI MAN U

DIRISHA la usajili limefunguliwa rasmi tangu, Juni 10, mwaka huu na litafungwa Septemba Mosi mwaka huu ikiwa ni wakati muhimu hasa kwetu kama Manchester United kwa kuhakikisha tunafanya maboresho.

Jana Manchester United ilithibitisha rasmi kuachana na nyota wake 11 huku nje ya hao kuna wengine pia wanaweza kuondoka kikosini hapo.

 Katika nyota ambao imethibitisha kuachana nao wa kikosi cha kwanza ni pamoja na Paul Pogba, Jesse Lingard, Edinson Cavani, Juan Mata na Nemanja Matic ambao wote mikataba yao imemalizika.Huku kipa Lee Grant yeye akistaafu soka.Lakini nyota wengine watano ni kutoka akademi ya Man United ambao nao wameondoka kikosini hapo.

 Wakati hao wakithibitiswa kuondoka nyota wengine ambao wanatajwa kuwa huenda wakaondoka hapo ni Anthony Martial, Eric Bailly na Phils Jones huku Aaron Wan-Bissaka yeye akiwekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa.

 Kumbuka kuwa tayari kocha mpya wa Man United Erik ten Hag ametinga ndani ya kikosi hicho na kuanza kazi hasa akiweka mipango kipindi hiki cha usajili huku vita ya usajili ikionekana kuwa kali ndani ya Ulaya.

 Lakini tunaamini kuwa Ten Hag atafanya usajili kwa umakini mkubwa na sio kwa kukurupuka kwani Man United kwa sasa inahitaji kujengwa upya ili kuwa bora na kuanza safari ya kusaka mataji baada ya kuwa na ukame kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

 Wachezaji ni wengi ambao Man United imekuwa ikihusishwa nao kwenye usajili ambao unaendelea kwa sasa ndani ya Ulaya.

 Kumbuka kuwa Man United ina kazi kubwa ya kukisuka upya  kikosi chake katika maeneo yote.

 Man United tunahitaji straika bora  ambaye atakuwa na uwezo wa kufunga mabao na ambaye atakuwa kwa muda mrefu ndani ya timu akishirikiana na mkongwe Cristiano Ronaldo (37) pamoja na Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bruno Fernandes ambao wamekuwa wakicheza maeneo ya mbele kwani Martial ni kama bado mambo ni magumu na hakuna asilimia 100 kama United wataendelea naye kwani anaweza kuuzwa kutokana na kushindwa kuwa na kiwango cha mwendelezo hata alipotoka kwenda kwa mkopo Sevilla alishindwa kutamba akiwa huko.

 Hivyo kama tutapata straika imara na kiungo mshambuliaji itakuwa ni jambo zuri na straika aina ya Darwin Nunez angefaa sana lakini sasa United imepata upinzani mkubwa kutoka kwa Liverpool ambao wanatajwa wapo njiani kumaliza dili la straika huyo raia wa Uruguay.

 Lakini pia eneo lao la ulinzi limeonekana kuwa ni tatizo kubwa licha ya Raphael Varane kusajiliwa msimu uliopita,ila mambo yaliendelea kuwa magumu na nyota huyo akitumia muda mwingi kuuguza majeraha, japo Harry Maguire na Victor Lindelof kuwepo mambo yalikuwa hayasomeki na msimu huu wa 2021/22 tukiweka rekodi mbovu tukifunga mabao sawa na yakufungwa.

 Hivyo tunahitaji beki bora wa kati kuja kuongeza nguvu na hata upande wa kulia sababu Wan-Bissaka atauzwa, lakini kumbuka tunahitaji kiungo mkabaji ndiyo maana Man United imekuwa ikikomalia dili la Frenkie De Jong wa Barcelona.

 Ten Hag anatakiwa kujua kuwa na ana kazi kubwa kwa kuhakikisha  anaweka mambo yake vizuri ili kuwa na kikosi ambacho kitaleta ushindani ndani ya Premier League msimu ujao wa 2022/23, baada ya safari hii kusuasua.

 Ni wazi kuwa Man United ni kama inaanza upya kwenye kujipanga na hivyo dirisha hili wanatakiwa kulitumia vyema kwa kufanya usajili makini ambao utaweza kuibeba timu na wasipoteze fedha nyingi kwa ajili ya wachezaji ambao hawatakuwa msaada kwa timu.

WE ARE UNITED