KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Hitimana Thierry, amefunguka kuwa kasi waliyoanza nayo wapinzani wao, Yanga na mabao wanayofunga, imekuwa ikiwaongezea presha kubwa ya kuhakikisha wanapata matokeo katika mechi zao.Simba imepoteza pointi nne katika mechi tano ilizocheza, ikiwa imeshinda tatu na sare mbili.
Ilianza kwa suluhu dhidi ya Biashara United kabla ya kuifunga Dodoma Jiji bao 1-0, kisha ikaifunga Polisi Tanzania bao 1-0, halafu ikasuluhu na Coastal Union kabla ya kuichapa Namungo kwa bao la ‘usiku’.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Hitimana alisema kuwa kasi ya wapinzani wao imekuwa ikiongezeka kadiri muda unavyokwenda kutokana na kutengeneza mabao hali inayoongeza presha kubwa ndani ya kikosi chake kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri kwenye mechi za karibuni licha ya kuamini ni suala la mpito kwao.
“Ukweli tumekuwa na presha kubwa kutokana na matokeo mabaya timu imekuwa ikitengeneza katika mechi ambazo tumecheza hadi kufikia wakati huu na hii ni kwa kuwa wapinzani wetu wameanza na kasi kubwa ya matokeo mazuri kitu ambacho tunakipigania ili kuweza kurejea kwenye mstari ambao tulikuwepo au tunaamini tunaweza kuwepo kwa kuwa hata nusu ya ligi bado haijafikiwa.
“Unajua hii imechangiwa na matokeo ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo imepelekea wenzetu tuliokuwa nao kuondolewa, sasa ile picha bado imekuwa changamoto ya timu kuweza kurejea kwenye ubora wake ingawa bado naamini itakuwa ni suala ambalo litaturudisha kupambana na wapinzani licha ya ubora ambao wapo nao,” alisema Hitimana.