KUMBE YANGA BADO INAJITAFUTA

BAADA ya Yanga kujikusanyia pointi 15 katika michezo mitano ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amewataka mashabiki wao wasiwe na hofu kwani huu ni mwanzo tu, mazuri zaidi yanakuja.

 

Yanga imekuwa kwenye kiwango bora msimu huu ambapo imefanikiwa kuweka rekodi ya kushinda mechi tano za mwanzo kwenye Ligi Kuu Bara kitu ambacho timu zingine zimeshindwa kufanya.

Akizungumza na Spoti Xtra, Nabi alifichua kwamba, alitumia muda mrefu kuitengeza Yanga ambayo haya ni matokeo madogo tu kati ya yale aliyoyapanga katika muda wote tangu atue kikosini hapo.

“Tunashukuru tumeweza kupata matokeo mazuri, Yanga ni timu kubwa Afrika, wakati nimefika hapa nilihitaji muda kidogo kukisoma kikosi na tayari nimefanikiwa kwa asilimia kubwa.

“Bado sijaridhika kwa namna kikosi changu kinavyocheza licha ya kupata matokeo bora kwenye kila mchezo ambao tumeshuka dimbani, tunahitaji kuongeza ufanisi zaidi ili tufikie pale tunapopataka.

“Tunatengeneza nafasi nyingi ambazo tunashindwa kuzitumia, tunapaswa kulifanyia kazi hilo kwani tunahitaji kufunga mabao mengi zaidi ili tujiweke kwenye mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.

“Mashabiki waendelee kuwa watulivu, muda si mrefu wategemee kuiona ile Yanga ambayo wanatamani kuiona kila siku.

“Tunahitaji kutwaa ubingwa, hivyo ni lazima tupambane kupata pointi tatu katika kila mchezo na ili tuweze kulifanikisha hili ni lazima tuyafanyie maboresho mapungufu yote ambayo yanajitokeza kwenye kila mchezo ambao tumecheza,” .