WAKATI leo Mei 29 Coastal Union ikitarajiwa kutupa kete yake mbele ya Azam FC kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali, Kombe la Shirikisho, Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema kuwa Azam FC wana timu nzuri.
Mgunda ambaye ni Kocha Mkuu wa Coastal Union ameweka wazi kwamba anawaheshimu wapinzani wake na anaamini wataleta ushindani mkubwa lakini nao wanahitaji kushinda.
“Tunakutana na wapinzani wazuri ambao ni Azam FC ukitazama hawa wana timu nzuri na wana gari zuri ambalo wanalitumia hapo kuna utofauti ambao upo.
“Sisi tumeweza kufika hapa hilo ni jambo la kwanza kisha tunakweda kupambana kupata matokeo hilo linakuwa jambo lingine na tunaamini inawezekana.
“Kikubwa ni mashabiki wetu kuweza kujitokeza na kuona namna ambavyo tutafanya,tupo tayari na vijana wapo tayari kwa ushindani,” amesema Mgunda.
Gari la Azam FC limepewa jina la ndege inayotembea ardhini kutokana na thamani yake kuwa zaidi ya bilioni 5 na lipo moja ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Sheikh mri Abeid, Arusha.