WAKATI leo nyota wawili wa Yanga, Said Ntibanzokiza na Dickson Ambundo wakitarajiwa kuukosa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Simba mikoba yao inatarajiwa kuwa mikononi mwa Jesus Moloko.
Ni kwenye suala la mapigo ya mipira huru hasa kona ambapo kwenye mechi za hivi karibuni ni Ntibanzokiza alikuwa akitumika mara kwa mara na Ambundo kidogo.
Kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Geita Gold, Ntibanzokiza alipiga jumla ya kona 10 kwenye mchezo huo na kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya Kwanza Ambundo alipiga kona mbili.
Kutokna na nyota hao kutokuwepo leo ni wazi kwamba jukumu la mapigo ya kona litakuwa mikononi mwa Jesus Moloko winga kutoka DRC Congo ambaye amekuwa akipewa kazi hiyo pia kwenye mechi za ligi kama ambavyo alifanya kwenye mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza alipiga kona mbili kipindi cha kwanza ilikuwa dk ya 12 na 33.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara amesema kuwa wachezaji hao watazungumza na uongozi mara baada ya mchezo dhidi ya Simba kutokana na matatizo ya nidhamu.