MTIHANI mwingine wa kusaka pointi tatu kwa vigogo ndani ya ligi, Azam FC V Simba ni leo Uwanja wa Azam Complex kwa timu kuwa kwenye msako wa pointi tatu.
Macho na maskio kwa muda wa dk 90 utakuwa hapo kusubiri nini kitatokea,hapa tunakuletea kazi zitakavyokuwa:-
Mechi zao tano zilizopita
Azam FC ilikuwa kwenye mechi 5 za kazi msimu huu wa 2021/22 kila iliposhuka uwanjani kwa namna yoyote ile ilikuwa lazima kipa atakayekuwa langoni aokote mpira wavuni.
Kwenye dk 450 waliokota nyavuni mabao 8 na safu yao ya ushambuliaji ilifunga jumla ya mabao 6 na ni sare moja iliambulia, ushindi mchezo mmoja na kichapo mechi tatu.
Kwenye msako wa pointi 15 ilikusanya pointi 4 na kuyeyusha pointi 11, ilikuwa nyumbani kwenye mechi 2 na iliweza kuwa ugenini kwenye mechi 3.
Mwendo wao ulikuwa hivi:-Azam FC 1-2 Yanga,Geita Gold 2-2 Azam FC,Kagera Sugar 1-0 Azam FC,Azam FC 2-1 KMC na Mbeya City 2-1 Azam FC.
Simba mwendo wao
Simba katika mechi hizo ni tatu walikuwa ugenini na mbili walikuwa nyumbani, ilikuwa namna hii:-
Kwenye mechi tano ambazo ni dk 450 waliweza kufunga mabao 8 na ukuta wao uliruhusu jumla ya mabao tatu na ni mechi mbili wakiwa ugenini hawakufungwa wala kufunga.
Kwenye msako wa pointi 15 walisepa na pointi 9 na kuyeyusha pointi 6 jumlajumla.
Kisasi kulipwa kwa haki
Ni wakati wa kulipa kisasi kwa haki kwa kuwa Azam FC mchezo wa mzunguko wa awali uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Simba 2-1 Azam FC.
Hivyo mchezo wa leo utakuwa ni wa kulipa kisasi cha haki kwa kila atakayepata nafasi, Simba watakuwa wanapambana kulipa kisasi cha ngome hiyo kutunguliwa bao moja huku Azam FC wakiwa na hesabu za kulipa kisasi cha kufungwa mchezo wao uliopita.
Kicheko kwa mashabiki
Hesabu zinazidi kuwa ngumu kwa Azam FC kutokana na mwendo mbaya waliokuwa nao kwenye mechi za ligi huku Simba wao wakitafuta tabasamu la mashabiki ambalo limeanza kurejea kutokana na matokeo ya mechi mbili mfululizo za ushindi.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabiti amesema kuwa kushindwa kupata matokeo kwenye mechi zao zilizopita hawajazoea.
“Hatujazoea kupata matokeo mabaya hali inayofanya tuwe na msimu mbaya hata wachezaji hawajazoezoa hivyo kwa mchezo wetu dhidi ya Simba tunahitaji kupata matokeo mazuri,” .
Ahmed Ally, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa bado ligi haijaisha na ubingwa ni asilimia 50 kwa kila timu kitakachowapa nguvu ni matokeo.
“Tunazidi kuendelea kusaka ushindi kwenye mechi zetu na tunawaheshimu wapinzani wetu ikiwa ni pamoja na Azam FC lakini bado kuna suala la ubingwa wa ligi ukizingatia ligi haijaisha na kila mmoja ana asilima 50 kuweza kuutwaa,”.
Nyota zao kali uwanjani
Rodgers Kola kwa Azam FC ni mzuri kwenye kufunga akiwa ametupia mabao 7 na ametoa pasi mbili za mabao huku akianza kikosi cha kwanza mechi 13.
Ismail Kader katupia mabao 5 na pasi mbili za mabao ndani ya kikosi cha Azam FC
Kibu Dennis wa Simba katika ligi katupia mabao 6 na pasi 2 kwenye mechi 15 ambazo amecheza.
Meddie Kagere ni namba moja kwa kucheka na nyavu ndani ya Simba akiwa ametupia mabao 7 na pasi mbili za mabao.
Makipa na kazi zao
Kama ataanza Ahmed Salula huyu kacheza mechi 14 hajafungwa kwenye mechi 4 na katunguliwa mabao 14,ikiwa itakuwa ni Mathias Kigonya yeye kakaa langoni mechi 9 kafungwa mabao 10 na hajafungwa kwenye mechi 3.
Kwa upande wa Simba ikiwa ataanza Aishi Manula yeye kakaa langoni kwenye mechi 20 kafungwa mabao 10 na hajafungwa kwenye mechi 11, akigushwa Beno Kakolanya ameanza langoni mechi 3 hajafungwa.