“HAYA mafanikio tuliyoyapata SportPesa kwa kipindi cha miaka mitano tuliyoyaanza Mei 9, 2017, tumepanga kuyaendeleza zaidi ya hapa.
“Kikubwa tunataka kuona tunaendelea kuongoza hapa nchini katika uendeshaji kwa kuanzia mifumo mbalimbali ikiwemo kuweka uwazi kwa washindi na kisasa kabisa kutoka 20% hadi kufikia 40%.
“Tunataka akifikiria kucheza ubashiri, basi afikirie kucheza na SportPesa na sio makampuni mengine kama ilivyokuwa hivi sasa, kila Mtanzania akitaka kucheza ubashiri wake, basi anaanza na SportPesa.
“Hiyo itasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania, pia kuongeza kiwango cha fedha kitakachofikia Sh 1.5Bil kutoka Sh 200Mil tulizoanza nazo katika Jackpot ambayo imepanda na kufikia Sh 1.2Bil ambayo inashindaniwa hivi sasa.
“Wakati bonasi hiyo ikishindaniwa tunaandaa bomu jipya la kulilipua ambalo linakuja hivi karibuni, hivyo wanaocheza na SportPesa wajiandae.”
Huyo siyo mwingine ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi SportPesa, Tarimba Abbas ambaye alifanya mahojiano maalum na Spoti Xtra.
Inaelezwa SportPesa wameweka udhamini wa Sh 1Bil katika kila timu za Simba na Yanga ambayo kila mwaka wanazipatia klabu hizo kubwa na kongwe hapa nchini ambazo katika msimu ujao huenda zikaongezeka zaidi ya hizo.
WALIANZA KUPAMBANA NA MAKAMPUNI WALIYOYAKUTA
“Wakati tunaingia katika michezo hii ya kubashiri mwaka, 2017 tulikuta baadhi ya makampuni ambayo yalikuwa yakiongoza, lakini ninashukuru tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana nayo na kuwazidi.
“Hilo lipo wazi kabisa kati ya kampuni inayoongoza katika michezo ya ubashiri, basi SportPesa hivi sasa tunaongoza, kila Mtanzania hivi sasa anahitaja kampuni yetu.
“Haikuwa kazi ndogo kupambana kuhakikisha tunakua wa kwanza, hiyo ilitokana na sisi kuchezesha michezo hii kiuweledi na uwazi bila ya upendeleo wowote na hayo ndiyo yalikuwa malengo yetu ya kwanza, tunashukuru tumefanikiwa.
“Wakati tunakuja na hilo la kuchezesha kiuweledi na uwazi, tulileta wataalam mbalimbali kutoka Kenya, Afrika Kusini, Italia na kwingineko ambako waliifanya kampuni yetu kuwa bora.
MALENGO NA FAIDA WALIZOZIPATA SPORTPESA NDANI YA MIAKA MITANO
“Malengo tuliyoyapanga wakati tunaingia katika mchezo huu wa ubashiri, kitu cha kwanza kilikuwa ni kurudisha kile tunachokipata katika jamii.
“Hivyo Watanzania wengi wamekuwa wakishinda kupitia SportPesa, kushinda kwao kunaongeza kipato na kubadilisha maisha yao.
“Pia tumepanga kurejesha mchezo huu wa ubashiri kwa njia ya Online Cassino, hiyo kuhakikisha Watanzania wanabadili maisha yao kupitia SportPesa.
ASIMULIA JINSI WALIVYOZITOA KATIKA HALI NGUMU SIMBA, YANGA
“Udhamini wetu wa kwanza katika soka ulikuwa kwa klabu za Simba na Yanga mwaka 2017, kiukweli tulizikuta timu hizi zikiwa katika hali ngumu kiuchumi.
“Lakini baada ya udhamini wetu tulifanikiwa kuziokoa kwa kutimiza makubaliano yote tuliyokubaliana katika mikataba kwa miaka mitano tuliyoingia.
“Kiukweli kabisa hatukuwahi kuchelewa kutimiza makubaliano yetu katika mkataba.
“Tunajivunia katika hili, kwani unapofikia muda wa kuwalipa, basi tumekuwa tukifanya kwa wakati.
“Tulitimiza hayo yote kwa ajili ya kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea katika kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu ya kukuza mchezo huu wa soka.
WAJIVUNIA KUZILETA KLABU ZA EVERTON NA SEVILLA
“Tukiwa wadau wakubwa wa soka tuliokuwa na malengo ya kukuza mchezo huu, tulijitahidi kufanya vitu vikubwa vya kufikirisha ambavyo havitasahaulika kwa kuzileta klabu kubwa za Everton ya Uingereza na Sevilla ambayo ipo Hispania.
“Hakikuwa kitu kidogo kwetu, kupitia ujio wa klabu hizo kubwa za Ulaya kutoka SportPesa, ongezeko la watalii waliokuja nchini kutembea liliongezeka kwa kiasi kikubwa. Hiyo ni kati ya faida kubwa iliyoipata nchi.
“Hiyo ni moja ya faida kubwa ambayo Serikali iliipata kupitia sisi SportPesa ambao malengo yetu kuona nchi inapiga hatua kupitia mchezo wa soka.
“Pia ujio wa Sevilla na Everton umeongeza faida kubwa kwa Serikali, kwani tulitumia Sh 1.6bilioni katika ukarabati wa Uwanja wa Mkapa.
“Tulilazimika kupanda nyasi mara mbili tofauti wakati wa ujio wa Everton na baadae Sevilla, ukarabati huo ulichukua baadhi ya maeneo ambayo ni uwanjani kwa kuweka mchanga, nyasi za kisasa kutoka Ulaya ambazo zipo hadi hivi sasa zinatumika.
“Kufanya ukarabati katika vyumba vya kubadilishia nguo na kununua trekta zinazotumika hadi hivi sasa kwa ajili ya kupunguza nyasi za uwanjani hapo ambazo zote ni mali ya Serikali.
KUREJESHA SPORTPESA SUPER CUP
“Kikubwa kilichosababisha kutokuwepo na mwendelezo wa SportPesa Super Cup ambayo tuliyaanzisha mwaka 2017 ni Covid pekee kutokana na baadhi ya nchi kuathirika na virusi hivyo.
“Mashindano haya yalishirikisha timu za Simba, Yanga, Singida United, Mbao FC na timu nyingine kutoka Kenya ambazo ni Gor Mahia, AFC Leopards, Kariobangi Sharks, Kakamega Homeboyz na JKU ya Zanzibar.
“Hivyo tumepanga kuyarejesha upya kivingine katika miaka mingine inayofuatia, tunajipanga upya na mawazo mapya ya kuboresha mashindano haya.
MCHANGO WA SPORTPESA KIUCHUMI NA JAMII
“Tumeweka Sh 35Bil za uwekezaji hapa nchini mara baada tu ya kuanza uwekezaji kupitia michezo ya ubashiri.
“Kupitia uwekezaji huu, tumetoa ajira kwa Watanzania 104 na wakati tunaanza walikuwepo watu kutoka nje ya nchi sita, lakini hivi sasa wamebaki wawili pekee wengine wote Watanzania, siyo kitu kidogo kwetu SportPesa kukifanya. Kwani hakuna Kampuni ya ubashiri iliyotoa nafasi za ajira kama hii yetu.
“Pia katika kipindi hicho tumewalipa Watanzania zawadi ya Sh 344Bil ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. Wapo washindi mara sita wa Jackpot walioshinda Sh 200Mil- 300Mil. Pia wapo washindi wa Jackpot kubwa ya Sh 800Mil ambao walikuwa wawili waligawana Sh 400Mil kila mmoja. Hivyo jumla ya washindi wote walioshinda na SportPesa kwa kipindi hicho chote cha miaka mitano tumelipa Sh 63.3Bil.
CHANGAMOTO WANAYOKUTANA NAYO
“Ni mifumo ya ulipaji wa kodi iwe ya uwazi ili wachezaji wafaidike na wavutiwe kucheza michezo hii ya ubashiri, yawepo maoni ya kusikilizwa kwa makampuni haya ubashiri na mengine.
“Kwa mfano hivi sasa ipo Jackpot kubwa ya Sh 1.2Bil tuliyoitangaza ambayo hivi sasa inashindaniwa, basi wachezaji wajitokeza katika kucheza,” anasema Tarimba.