MAYELE AMPA JEURI MPOLE, ATOA TAMKO LA KUPAMBANA ZAIDI

STAA wa Klabu ya Geita Gold FC, George Mpole amesema kuwa siri iliyopo nyuma ya uwezo wake mkubwa wa kufunga kwenye ligi msimu huu ni ubora wa washambuliaji na wachezaji wakigeni ambao wamekuwa wakitesa kwenye ligi ya Tanzania.

Mpole alisema, wachezaji hao wamekuwa wakimpa chachu ya kuendelea kupambana zaidi akiwa uwanjani ili kuweza kupambania nao nafasi ya kufanya vizuri viwanjani na hiyo imekuwa moja ya siri zake za mafanikio.

Mpole ambaye kwa sasa ameungana na Fiston Mayele kwa kufunga mabao 12 kwenye ligi, aliongeza kuwa jambo lingine linalompa nguvu ni ongezeko la watu ambao wamekuwa wakifuatilia soka la Bongo kutoka nje ya nchi.

“Nafikiri ligi yetu kwa sasa imekua sana na inatazamwa nanchi nyingi za Afrika. Hivyo kwangu mimi na wachezaji wazawa tunaitumia hiyo kama nafasi ya kufanya vizuri zaidi ili tuonekane.

“Lakini pia hawa wachezaji wakigeni tunaocheza nao, wamekuwa na mchango mwingine kwetu. Kwani tumekuwa tukiwaangalia wanavyocheza na kufunga ili nasi tuwe bora kama wao viwanjani,” alisema.