WAKATI ikitajwa kwamba mabosi wa Simba wanalijadili jina la Shiza Ramadhan Kichuya kwenye usajili wao msimu ujao, baba mzazi wa kiungo huyo, Ramadhan Kichuya amebainisha kwamba, anataka kumuona kijana wake akijiunga na Yanga SC.
Baba Kichuya amesema mwanawe huyo atakuwa na wakati mzuri zaidi akiichezea Yanga na siyo Simba ambayo amekuwa na mapenzi nayo kwa muda mrefu.
Kichuya baada ya msimu huu kuonesha uwezo mzuri, ameonekana kuziingiza vitani Simba na Yanga kama ilivyotokea mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar na kufanikiwa kusaini Simba.
Kiungo huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto, aliwahi kuitumikia Simba kwa vipindi viwili tofauti akianza kujiunga na timu hiyo Julai 2016 akitokea Mtibwa, kabla ya kuondoka 2019 na kwenda Misri kucheza soka la kulipwa, kisha kurudi Simba Januari 15, 2020, mwanzoni mwa msimu wa 2020/21, akajiunga na Namungo alipo sasa.
Uwezo aliokuwa nao msimu huu akiwa na mchango wa mabao matano kati ya 28 yaliyofungwa na Namungo ndani ya Ligi Kuu Bara, akifunga matatu na kutoa asisti mbili, ndiyo uliowafanya vigogo hao kuanza kumjadili.
Lakini wakati Simba wakianza kumjadili, mabosi wa Yanga nao wameona nyota huyo anawafaa, hivyo nao wanamuhitaji katika kikosi chao msimu ujao.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kwamba: “Kutokana na ubora wa Kichuya alionao kwa sasa, viongozi wa Yanga wameanza kumjadili wakihitaji kumsajili kwa msimu ujao.
“Wakiwa wanamjadili, wamekuwa na hofu kwamba huenda yakatokea kama yale ya Ajibu (Ibrahim) baada ya kumuhitaji kwa mara ya pili, wanachama wakamkataa, hivyo bado suala lake lipo gizani, lakini kama mambo yakiwa sawa, basi Kichuya atavaa jezi ya Yanga msimu ujao.”
Akizungumza na Spoti Xtra, Baba Kichuya alibainisha kwamba: “Nimesikia kuhusu Simba kuhitaji kumrejesha nyumbani Kichuya, lakini hata Yanga kipindi cha nyuma nao walikuwa wanamuhitaji.
“Mimi ningetamani sana aende kucheza Yanga ambapo kuna ushindani mkubwa tofauti na Simba. Naamini akienda Yanga atafanikiwa zaidi kuliko kurudi Simba.”