UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kwamba wanaweza kufungwa kwenye mechi za ligi ila hilo haliwataondoa kwenye mpango wa kutwaa taji la Ligi Kuu Bara.
Kwenye msimamo Yanga ni namba moja ikiwa imecheza mechi 22 na kukusanya pointi 56 ikiwa haijapoteza mchezo zaidi ya kuambulia sare 5 na kushinda mechi 17.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa kwenye malengo ambayo wanayo hawajaweka suala la kutokufungwa ila suala la kuchukua ubingwa hilo lipo.
“Kwetu sisi suala la kufungwa hatujaweka kwenye malengo lakini suala la kuchukua ubingwa hilo lipo hivyo tunajua tunaweza tukafungwa lakini haina maana kwamba hatutachukua ubingwa.
“Kwa mfano hata ingetokea tukafungwa na Simba kwenye mchezo wetu wa ligi tungeumia lakini tungerudi kwenye lengo letu kubwa ambalo ni kutwaa ubingwa hapo wachezaji wangetambua kwamba bado malengo hatujapoteza zaidi ya mchezo pekee,” amesema Bumbuli.