AHMED Ally, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano ndani ya Simba amesema kwa sasa hawafikirii mchezo wao dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Aprili 30,2022.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu zote kuwa na uhitaji wa pointi tatu muhimu za mchezo huo wa ligi.
Ally amesema wanatambua mchezo huo upo ila hawafikirii sana kuhusu mchezo huo mpaka pale watakapopata muda wa kutulia.
“Tumeweza kuwa kwenye mashindano makubwa na kutolewa kwenye hatua ya robo fainali sasa akili zetu sio kwenye mechi yetu dhidi ya Yanga hiyo hatuifikirii.
“Tumekuwa kwenye hatua ya tofauti na hatuwezi kuifikiria mechi yetu dhidi ya Yanga kwa muda mrefu ni wakati wetu kuangalia namna ambavyo tunaweza kuwa imara zaidi kwa wakati ujao kimataifa kisha hapo tutaanza kufikiria kuhusu Yanga,” amesema.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Simba na Yanga zilitoshana nguvu kwa kukamilisha dk 90 bila kufungana.
Kwenye msimamo, Yanga ipo nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 20 inatarajiwa kukutana na Sima iliyo nafasi ya pili na pointi 41.