SIMBA NDANI YA DAR,KANOUTE,INONGA,MANULA NDANI

WACHEZAJI wa Simba pamoja na viongozi usiku wa kuamkia leo Aprili 26 wameweza kurejea salama Tanzania wakitokea nchini Afrika Kusini ambapo walikuwa na mchezo wa hatua ya robo fainali.

Ilikuwa ni robo fainali ya pili na ya maamuzi ambapo Simba iliweza kuambulia kichapo cha bao 1-0 ugenini.

Kwa kuwa walikuwa wameshinda nao pia bao 1-0 Uwanja wa Mkapa ngoma ilibidi ipigwe penalti ili kumpata mshindi atakayetinga hatua ya nusu fainali.

Orlando Pirates waliweza kushinda kwa penalti 4-3 na kuifungashia virago Simba inayonolewa na Kocha Mkuu Pablo Franco.

Wachezaji pamoja na viongozi wamepokelewa kwa shangwe ikiwa ni pamoja na beki wa kazi chafu Henock Inonga pamoja na kiungo Sadio Kanoute.

Pia kipa namba moja Aishi Manula, Shomari Kapombe,Mohamed Hussein pamoja na Jonas Mkude ni miongoni mwa mastaa ambao walipokelwa kwa shangwe na mashabiki.

Ahmed Ally, Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Simba naye amepokelewa kwa shangwe kisha akacheza na mashabiki kabla ya  kutoa neno la shukurani.