SIMBA YATAKA USHINDI WA MAPEMA,YATAJA WATAKAOMALIZA KAZI

KOCHA Mkuu wa Simba, Mhispania, Pablo Franco Martin anaamini mchezo wa marudiano dhidi ya Orlando Pirates utakuwa mgumu lakini ataingia uwanjani kwa mbinu tofauti ya kupata bao la mapema ndani ya dakika 10 hadi 15 za mwanzoni.

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana kesho Jumapili katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Johannesburg, Afrika Kusini.

Katika mchezo wa kwanza ambao ulipigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ilifanikiwa kuwafunga Pirates bao 1-0 ambalo lililifungwa na Shomari Kapombe kwa njia ya penalti.

Kama Simba wakipata bao la mapema, maana yake Orlando watatakiwa kufunga mabao matatu ili wafuzu, kutokana na Simba kutumia faida ya bao la ugenini.

Pablo amesema kuwa anaheshimu ubora wa Pirates ambao wamekamilika katika kila nafasi, lakini hiyo haimfanyi awaogope na badala yake atawapa mbinu za ushindi vijana wake zitakazowawezesha kupata ushindi ugenini.

Pablo amesema kuwa walivyoingia katika mchezo uliopita hapa nyumbani, ni tofauti watakavyocheza katika mchezo wa marudiano wakiwa ugenini.

Aliongeza kuwa katika mchezo huo, anataka kuona vijana wake wakipambana na ndani ya dakika 10 hadi 15 za mwanzo, wawe wameshapata bao la kuongoza litakalowavuruga Pirates.

“Lipo wazi kabisa tutakuwa na mchezo mgumu ugenini kwa Pirates, kwani wapinzani wetu wataitumia vizuri faida ya mashabiki wao watakaoingia uwanjani kuwasapoti kwa lengo la kutuvuruga.

“Lakini hiyo haitufanyi tuiogope Pirates, badala yake kama kocha nitakaa na wachezaji wangu kuwatengeneza kisaikolojia na kuwapa mbinu mbadala zitakazotuwezesha kupata pointi tatu.

“Katika mchezo huo tutaingia na mpango wetu ambao ni kupata bao la kwanza la kuwaongoza ndani ya dakika 10 hadi 15 kwa lengo la kuwaongezea presha na kuwavuruga, ninaamini tutafanikiwa katika hilo.

“Ninaamini hilo linawezekana kama washambuliaji wangu Sakho (Ousmane), Mugalu (Chris) na Banda (Peter) watafuata maagizo yangu na kutumia vema kila nafasi ya kufunga watakayoipata,” amesema Pablo.