MTAMBO WA MABAO SIMBA KUIKOSA ORLANDO PIRATES

MTAMBO wa mabao ndani ya kikosi cha Sima, Bernard Morrison kwenye mechi za kimataifa anatarajiwa kuukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Orlando Pirates.

Ni mabao matatu ambayo amefunga na kutoa pasi tatu na amesababisha penalti moja hivyo kahusika kwenye mabao 7 kati ya 17 ambayo yamefungwa na timu hiyo  katika mechi za kuanzia hatua ya Ligi ya Mabingwa, mtoano, makundi na sasa hatua ya robo fainali.

Alifunga mabao mawili mbele ya Red Arrows kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa  na alitoa pasi moja ya bao katika ushindi wa mabao 3-1.

Alitupia bao moja mbele ya USGN ugenini akitokea benchi kwa pasi ya mshikaji wake Shomari Kapombe aliyepewa jukumu la kupiga kona.

Pasi mbili alitoa kwenye mchezo dhidi ya USGN uliochezwa Uwanja wa Mkapa na mabao yalifungwa na Sadio Kanoute pamoja na Chris Mugalu.

Pia kwenye mchezo dhidi ya Orlando Pirates alisababisha penati moja iliyofungwa na Shomari Kapombe baada ya kuchezewa faulo ndani ya 18.

Simba inakibarua cha kusaka ushindi Aprili 24 mbele ya Orlando Pirates ukiwa ni mchezo wa ngwe ya pili utakaoamua mshindi atakayetinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Meneja wa Kitengo cha Habari Simba, Ahmed Ally aliliambia Championi Jumatano kuwa watamkosa Morrison kwenye mchezo wa pili kutona na kuwa na matatizo na ofisi za uhamiaji nchini Afrika Kusini.