SIMBA YATAJA MECHI NGUMU KIMATAIFA

MOHAMED Hussein Zimbwe Jr, beki wa kazi ngumu ndani ya kikosi cha Simba amesema kuwa mechi ambayo kwenye hatua ya makundi kwao anaamini ilikuwa na ushindani mkubwa ni ile dhidi ya ASEC Mimosas.

Kwa sasa Simba imeweza kutinga hatua ya robo fainali na inasubiri kujua itamenyana na timu ipi baada ya droo kupangwa ya Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.

Leo Aprili 5 Simba itakuwa na kazi ya kusubiri nani atapangiwa kucheza naye kwenye hatua ya robo fainali baada ya kuweza kufikisha pointi 10 ikiwa sawa na RS Berkane kutoka kundi D.

Zimbwe ambaye ni nahodha msaidizi wa Simba amesema kuwa mechi zote zilikuwa ni ngumu kwenye hatua ya makundi kutokana na ushindani uliokuwepo ila dhidi ya ASEC ilikuwa ni ngumu zaidi.

“Ikiwa utaniambia kwa upande wangu mechi zote zilikuwa ngumu kuweza kupata ushindi na hata zile ambazo tulipoteza lakini mbele ya ASEC ilikuwa ni ngumu katika kusaka ushindi.

“Hawa ukitazama tulikutana nao nyumbani tukashinda na tulipowafuata ugenini ikawa tofauti hivyo ni moja ya timu iliyoleta ushindani mkubwa.

“Tunashukuru kwa hatua ambayo tumeweza kufika,shukrani kwa mashabiki pamoja na benchi la ufundi kwa kuwa wamekuwa nasi kwenye kila matokeo,”

Nyota huyo alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya USGN ilikuwa dk 60 kwenye harakati za kutimiza majukumu yake lakini kwa sasa anaendelea vizuri.