ZILITEMBEZWA KADI ZA NJANO KWA MKAPA,CHEKI ILIVYOKUWA

WAKATI ukurasa ukifungwa kwa Yanga kuimaliza KMC Uwanja wa Mkapa ulipigwa mpira wa darasani huku wachezaji wakitembezeana mikasi ya kishkaji katika msako wa pointi hizo.

Ubao ulisoma Yanga 2-0 KMC ilikuwa ni Machi 19 na waliofanya iwe hivyo ni Matheo Anthon dk ya 39 kwa bao la kujifunga na Djuma Shaban ilikuwa dk ya 51.

Weka kando suala la Yanga kuwa namba moja na pointi 48 hapa Championi Jumatatu linakuletea msako ulivyokuwa kwenye mchezo huo:-

Zilitembezwa kadi za njano

Dakika 45 za mwanzo timu zote zilicheza kwa hesabu kubwa huku kila mmoja akiwa anatafuta pa kutokea na mwamuzi wa kati Hery Sasii hakutoa kadi yoyote mfukoni.

Kipindi cha pili hao KMC walicharuka walitembeza mabuti kama yote na walikutana na kadi za njano ambapo jumla wachezaji watano walionyeshwa kadi za njano.

Abdul Hassan huyu alikuwa benchi lakini alipoingia alionyeshwa njano dk 87 baada ya kumchezea faulo Fiston Mayele kama ambavyo ilikuwa kwa Masoud pia dk ya 83 naye alionyeshwa kadi ya njano.

Hassan Kessy ambaye alikuwa kwenye ubora pia alionyeshwa kadi ya njano dk ya 65, Charlse Ilanfya naye alionyeshwa kadi ya njano dk ya 90 na nyota mwingine ni Kenny Ally dk ya 61 alimchezea faulo Dickson Job.

Huyu Chico kumbe mkorofi

Chico Ushindi alikuwa ni mkorofi kwenye mchezo wa juzi ambapo alimtembezea kiwiko nyota wa KMC, Emmanuel Mvuyekule ilikuwa dk ya 48 lakini mwamuzi hakuweza kuliona hilo tukio.

Kwenye mchezo huo aliweza kutoa pasi moja ya bao ilikuwa ni kwa Djuma Shaban baada ya kupiga kona ilikuwa dk ya 51.

Kaseja na Diarra mikono ya dhahabu

Licha ya Juma Kaseja kufungwa mabao mawili hakuna namna anastahili pongezi kwa kuwa alifanya kazi kubwa kuokoa le michomo ya Mayele ambaye alikuwa anahitaji kutetema ilikuwa dk ya 45 na 76 pia Chico alipiga mashuti mawili yaliishia mikononi mwa Kaseja ilikuwa dk ya 10 na 29 kwa Yanick Bangala ilikuwa dk ya 10 huku Djuma Shaban alifanya hivyo dk ya 13.

Diarra ilikuwa ni siku nzuri kwake kazini kwa kuwa lile shuti la Matheo Anthon dk ya 27 ilibaki kidogo libadili usomaji wa ubao pamoja,shuti la Awesu Awesu dk ya 76, Hassan Kabunda dk ya 80 na Ilanfya ilikuwa dk ya 81.

Wazee wa kujenga vibanda

Vibanda kwa Yanga alikuwa ni Mayele ambaye alinaswa kwenye mtego wa kuotea ilikuwa dk ya 34 na kwa upande wa KMC alikuwa ni dk ya 56 kwa Kabunda.

Wazee wa mikasi

Feisal Salum kiungo huyu wa Yanga alikuwa miongoni mwa nyota wa kwanza kucheza faulo ilikuwa dk ya 2 alimtembezea mkasi Sadala Lipangile, Djuma Shaban alimchezea faulo Kabunda ilikuwa ni dk ya 64.

Ilanfya alikuwa na lake alimtembezea mikasi Bangala ilikuwa dk ya 74 pia Kenny Ally yeye alikuwa na Job alifanya hivyo dk ya 61.

Makipa wote KMC ngoma droo

Makipa wote wa KMC Kaseja na Farouk Shikalo mbele ya Yanga wote wametunguliwa mabao mawilimawili, alianza Shikalo Uwanja wa Majimaji Songea kisha akamaliza Kaseja Uwanja wa Mkapa.

Kwenye msako wa pointi sita mbele ya Yanga KMC wameambulia 0.