MALI za mmiliki wa Klabu ya Chelsea na bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich zimezuiliwa rasmi na Serikali ya Uingereza kuanzia, Machi 10, 2022 kama sehemu ya kuwatia kitanzi matajiri wote wa Kirusi ambao wanahusishwa na kuwa na ukaribu na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Abramovich anaingia kwenye orodha ya mabilionea saba wa Urusi waliowekewa vikwazo ambapo wengine ni Oleg Vladimirovich Deripaska, Igor Sechin, Andrey Kostin, Alexei Miller, Nikolai Tokarev na Dmitri Lebedev.
Hatua hii ni mwendelezo wa vikwazo vya kiuchumi anavyowekewa Rais wa Urusi, Vladimir Putin na washirika wake kutokana na hatua ya majeshi ya nchi hiyo kuivamia Ukraine na kuendesha mashambulizi makali yaliyoingia wiki ya tatu sasa.
Mbali na kumiliki Klabu ya Soka ya Chelsea, Roman Abramovic anayekadiriwa kuwa na utajiri wa kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 12.3, pia anajihusisha na biashara nyingine mbalimbali, akimiliki makampuni makubwa ya nishati, kilimo, sekta za kibenki na uuzwaji na ununuaji wa nyumba na mashamba, real estates.
Miongoni mwa kampuni zinazomilikiwa na Abramovich ni Millhouse ambayo inajihusisha na usimamizi wa mali za Abramovich alizowekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mafuta katika kampuni ya Gazprom Neft ya Urusi, huduma za kifedha na benki, sekta ya kilimo lakini pia uwekezaji katika sekta ya umeme.
Abramovich mwenye uraia wa nchi tatu tofauti, Urusi, Israel na Ureno anatajwa kuwa mshirika wa karibu na rafiki mkubwa wa Rais Vladimir Putin.
Katika vikwazo alivyowekewa, timu ya soka ya Chelsea aliyokuwa akiimiliki kabla ya hivi karibuni kutangaza kutaka kuiuza, itaathirika vibaya na vikwazo hivyo ambapo kuanzia Machi 10, haitaruhusiwa tena kuuzwa.
Kutokana na mali za Abramovich kushikiliwa, Klabu ya Chelsea pia itakuwa chini ya uangalizi maalumu wa Serikali ya Uingereza na itajiendesha kwa kibali maalum huku shughuli zote za kiundeshaji zikiendelea kwa uratibu wa Wizara ya Utamaduni, Habari na Michezo.
Waziri wa wizara hiyo, Nadine Dorries amesema amewatoa hofu wafanyakazi wa timu hiyo kwamba itaendelea kuendeshwa kama kawaida na mishahara kwa wafanyakazi italipwa kama kawaida huku pia ratiba za mashindano zikiendelea kama zilivyopangwa.
Sambamba na hilo, Nadine amethibitisha kuwa maamuzi hayo lazima kwa namna moja au nyingine yatakuwa na madhara kwa Klabu ya Chelsea pamoja na mashabiki wake kwa jumla kwa sababu hakuna ruhusa ya kuuza au kusajili mchezaji yeyote kuanzia sasa wala kumuongezea mkataba mchezaji yeyote wa Chelsea.
Klabu haitaruhusiwa kuuza bidhaa yoyote ile kuanzia sasa na kuendelea na tayari maduka ya klabu yameshafungwa ambapo pia klabu haitaruhusiwa kuuza tiketi yoyote kuanzia sasa na kuendelea.
Mbali na hayo, pia Roman Abramovich amepigwa marufuku kufanya miamala ya fedha na watu binafsi na wafanyabiashara wa Uingereza huku pia akipigwa marufuku ya kusafiri.