BILIONEA WA UINGEREZA ATAKA KUINUNUA CHELSEA

BILIONEA kutoka nchini Uingereza na shabiki mkubwa wa Chelsea, Nick Candy amethibitisha kuwa na nia ya kutaka kuinunua Klabu ya Chelsea ambayo imewekwa sokoni na mmiliki wake, bilionea kutoka Urusi, Roman Abramovic.

Bilionea Candy ameweka mezani ofa ya kiasi cha paundi bilioni 2.5 pamoja na nyongeza ya paundi bilioni 1.5 kwa ajili ya matengenezo ya Uwanja wa Stamford Bridge, kitu ambacho matajiri wengine waliojitokeza wameshindwa kukifanya.

Candy mwenye umri wa miaka 49, ni shabiki mkubwa wa Chelsea na alianza kuishabikia timu hiyo akiwa na umri wa miaka minne huku kila msimu akiwa na tiketi za msimu mzima za kutazama mechi za Chelsea.

Msemaji wa Candy amesema: “Nick Candy kwa sasa anaangalia baadhi ya masuala kwa ajili ya kuinunua Chelsea. Ofa yoyote lazima tutaungana na kampuni nyingine na tupo makini na nia ya kuungana na wenzetu wa kimataifa.”

Ikumbukwe kuwa Roman Abramovic alisema tarehe ya mwisho ya kupokea ofa kwa ajili ya kuiuza Chelsea ni Machi 15, mwaka huu.