MZUNGUKO wa pili unazidi kumeguka taratibu ni kama vile ambavyo mzunguko wa kwanza ulianza kwa msimu wa 2021/22 hasa kwa timu kusaka ushindi.
Ipo wazi kwamba mzunguko wa maamuzi huwa huu wa pili kwa kuwa kile ambacho unakivuna wakati huu utapata majibu yake mwisho wa msimu.
Zile ambazo zipo nafasi za kushuka daraja wakati mwingine huwa zinabaki hapo mpaka msimu utakapoisha pale zinaposhindwa kuzinduka.
Ukweli ni kwamba wakati huu wa mwanzo wa mzunguko wa pili ni muda wa kupiga hesabu za nafasi ambayo timu inahitaji kuwa pamoja na sehemu ambayo inahitaji kukamilisha kwa msimu huu.
Tunaona kwamba kila leo timu zinaposhuka uwanjani zinapambana kusaka ushindi hili ni jambo kubwa na muhimu kwa kuwa hakuna anayeweza kushinda bila kujituma.
Mzunguko huu huwa unakuwa ni mgumu mwanzo mwisho kwa kuwa yule ambaye atapoteza mchezo huwa inakuwa rahisi kuondoka kwenye reli.
Ushindi popote hilo linaonekana kwa sasa hasa ukitazama namna ambavyo timu zinapata ushindi iwe ni nyumbani ama ugenini.
Polisi Tanzania, Coastal Union ni mfano wa timu ambazo zmeanza mzunguko wa pili kwa kushinda ugenini tena kwenye mechi ambazo zilikuwa na ushindani mkubwa.
Azam FC walipoteza mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani na Polisi Tanzania walishinda ugenini kwenye mchezo wa mzunguko wa pili mbele ya Azam FC na Coastal Union ilishinda mbele ya KMC.
Kila mmoja ambaye anaingia uwanjani kwa sasa ni lazima awe na uhakika wa kupata pointi tatu basi ni lazima ajipange sawasawa kwa kuwa hakuna timu ambayo haina hesabu ya kupata pointi tatu.
Hakuna mwenye uhakika wa kushinda mechi zote ikiwa hatafanya maandalizi mazuri na hakuna ambaye anaweza kushindwa ikiwa atakuwa na maandalizi mazuri.
Kinachobeba matokeo uwanjani na maandalizi mazuri kisha wachezaji kutumia nafasi wanazozipata uwanjani kunafuata kwa kuwa ushindi lazima upatikane kwa mabao kufungwa.
Wale ambao wanadhani bingwa atakuwa fulani kwa sasa waweke kando suala hilo na kuwekeza nguvu kwenye maandalizi kisha ubingwa utakuja.
Ipo wazi msimu lazima utakwisha kwa namna yoyote lakini suala la kusema kwamba fulani atakuwa bingwa wakati ligi inaendelea haipo sawa.
Iwe na Prisons, Mbeya City, Mbeya Kwanza mpaka Coastal Union bado wana nafasi ya kufanya vizuri na kurekebisha makosa ambayo waliyafanya mzunguko wa kwanza.
Geita Gold na Mbeya Kwanza hizi zinatambua kwamba Championship huko mwendo wake ni nguvu mwanzo mwisho kusaka ushindi hivyo hawafikirii kurejea tena huko.
Ila hata iweje zipo timu ambazo zitashuka na zitashiriki Championship msimu ujao njia ni moja yakuweza kuepuka hali hiyo mapema ni kujituma na kushinda mechi za nyumbani na ugenini.