SIMBA KURUDI KUJIPANGA UPYA KUWAKABILI BERKANE

BAADA ya kikosi cha Simba kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesema kuwa watashinda mechi ambazo watacheza nyumbani.

Kichapo hicho cha mabao mawili kinaifanya Simba kubaki na pointi 4 kibindoni huku RS Berkane ikifikisha pointi 6 na ni namba moja kwenye msimamo wa kundi D.

Kocha Pablo amesema:”Tumepoteza lakini katika michezo mitatu tumekuwa timu pekee ambayo ilipata alama ugenini.

“Tuna michezo miwili nyumbani, malengo yetu kwa sasa ni kushinda michezo hiyo na kujaribu kutafuta alama ugenini.”

Leo Simba inatarajiwa kurejea Dar kwa ajili ya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Bara na mchezo wao ujao ni dhidi ya Biashara United ya Mara.

Mchezo wao ujao kimataifa na RS Berkane unatarajiwa kuchezwa Machi 13 itakuwa Uwanja wa Mkapa.

Ikumbukwe kwamba kwenye mchezo uliochezwa nchini Morocco safu ya ushambuliaji ya Simba ilikwama kupiga shuti ambalo lililenga lango kati ya yale mawili ambayo walipiga baada ya dakika 90.

Mabao ya Adam Ba na El Bahri yaliweza kubadili upepo kwenye kundi D na kuwapa pointi 3 RS Berkane.