KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ametoa majukumu mazito kwa wachezaji wa timu hiyo, akiwemo kinara wa mabao, Fiston Mayele kwa kuhakikisha wanatupia mabao ya kutosha katika mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar kwa lengo la kuendelea kuongoza ligi.
Nabi ametoa kauli hiyo baada ya kurejea kwa ligi kufuatia kumaliza mechi za Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) huku wakiwa na kumbukumbu za matokeo ya suluhu katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mbeya City kabla ya ligi kusimama kupisha Shirikisho.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 14, ikishinda 11 huku ikiwa imetoka sare tatu. Ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi hadi sasa kwenye ligi huku ikitarajiwa kuivaa Mtibwa Sugar Jumatano
ijayo, Manungu.
Nabi amesema kuwa wanarejea kwenye ligi wakiwa na lengo moja la kuhakikisha wanapata matokeo ya ushindi katika mchezo wao ujao dhidi ya Mtibwa ili kuendelea kuongoza ligi hiyo, hivyo
amewataka kupambania matokeo ya uhakika katika mchezo huo.
“Tunarejea kwenye ligi baada ya mapumziko ya kucheza Kombe la FA, tunaelekea kucheza na Mtibwa Sugar katika mchezo mgumu wa ugenini ambao ni wazi tunahitaji kupata matokeo mazuri kwa hali yoyote ili kuendelea kubakia juu kuongoza ligi, kwa matarajio yetu msimu huu ni ubingwa ila presha ya ushindani imekuwa juu kutokana na wapinzani wetu kujipanga vizuri.
“Kila mchezaji kwa sasa anajua jukumu lake kuelekea kwenye mchezo huu mkubwa ambao matokeo kwetu ni jambo
la lazima, ukiangalia safu ya ushambuliaji tumekuwa na maongezi ya mara kwa mara kuhakikisha tunafikia
malengo ya kushinda katika kila mchezo, ingawa siyo kazi nyepesi,” amesema.
Chanzo:Chanzo Spoti Xtra