KIUNGO wa Azam FC, Tepsi Evance amemfunika nyota wa Namungo FC, Obrey Chirwa kwa vitendo katika suala la kutoa pasi za mwisho ndani ya ligi huku akiingia kwenye anga za Clatous Chama ambaye anatetea tuzo yake ya kiungo bora.
Chirwa ana pasi tatu za mabao pia anashikilia rekodi ya kutoa pasi zaidi ya moja kwenye mchezo mmoja alifanya hivyo mbele ya Geita Gold, Septemba 27,2021 Uwanja wa Ilulu,Lindi.
Tepsi yeye hana makuu mwendo wake ni wa mojamoja na ni kinara wa pasi za mwisho ndani ya ligi akiwa ametoa jumla ya pasi nne na ametupia mabao mawili na kumfanya ahusike kwenye mabao sita kati ya 20 yaliyofungwa na Azam FC.
Mbele ya Geita Gold alitopa pasi moja ya bao kwa mguu wake wa kulia,alitoa pasi ya pili kwa mguu wa kushoto mbele ya Simba, alitoa pasi ya tatu mbele ya Tanzania Prisons kwa mguu wa kushoto na pasi yake ya nne alitoa mbele ya Dodoma Jiji kwa mguu wa kulia.
Alitupia bao lake la kwanza mbele ya Ruvu Shooting kwa mguu wa kulia, alitupia bao la pili mbele ya Prisons kwa mguu wa kushoto.Chama alitoa pasi 15 na alifunga mabao 8 na alisepa na tuzo ya kiungo bora msimu huu ametupia bao moja.