MAYELE LIMEMKUTA JAMBO HUKO

BAADA ya kuona mabeki wa timu pinzani wakimkamia kila wanapokuwa uwanjani, Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, amemtaka straika wake, Fiston Mayele kuhakikisha hakai na mpira mguuni kwa muda mrefu ili kujiepusha na kupata majeraha yatakayoigharimu timu.

Mayele ndiye straika tegemeo kwenye kikosi cha Yanga akiwa kinara wa mabao akifunga sita ndani ya Ligi Kuu Bara, huku wikiendi iliyopita akifunga bao pekee kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC na kufuzu 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

Kocha Nabi ambaye aliungana na Yanga Machi 2021, msimu huu amepania kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambapo hadi sasa ameiongoza timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo kwa kukusanya pointi 35 kwenye mechi 13 akishinda 11, sare mbili, hajapoteza.

Habari zimeeleza kuwa, kufuatia mwenendo mzuri wa Mayele katika safu ya ushambuliaji, Nabi amemtaka kuwa makini na wapinzani ambao akifanya mzaha, watamuumiza na kuigharimu timu.

“Kocha amemtaka Mayele kuwa makini zaidi awapo uwanjani ili kuepuka kupata majeraha ambayo yataigharimu
timu.

“Ukiangalia hivi sasa wapinzani wanawakamia sana wachezaji wetu, hivyo amemtaka kutokaa sana na mpira mguuni
na badala yake awe anaachia haraka akipewa pasi au afunge akiona kuna nafasi ya kufanya hivyo.

“Mbinu hiyo itamfanya hata yule mwenye nia ya kutaka kumuumiza kushindwa kufanikisha jambo lake,” kilisema chanzo hicho.

Nabi amesema kuwa kila mchezaji kwenye timu hiyo ana nafasi ya kucheza na jambo ambalo wanahitaji kwenye mechi zao ni ushindi.

Chanzo:Spoti Xtra