Klabu ya Barcelona imeendelea kujiimarisha kileleni mwa La Liga baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo mkali uliopigwa kwenye dimba la Metropolitano.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa, ambapo wenyeji Atletico walitangulia kufunga dakika ya 39 kupitia kwa Simeone, kabla ya Barcelona kusawazisha dakika ya 42 kupitia kwa Marcus Rashford.
Hata hivyo, mambo yalizidi kuwa magumu kwa Atletico baada ya Nicolas Gonzalez kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 45+7, hali iliyowaacha wakicheza pungufu kwa kipindi kizima cha pili.
Barcelona walitumia vyema nafasi hiyo na kufanikiwa kupata bao la ushindi dakika ya 87 kupitia mshambuliaji wao hatari Robert Lewandowski, akihakikisha timu yake inaondoka na alama zote tatu muhimu.
Katika mchezo mwingine, Real Madrid ilipata pigo baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Mallorca, matokeo yaliyoipa Barcelona nafasi nzuri zaidi ya kujikita kileleni.
Kwa ushindi huo, Barcelona imefikisha pointi 76 baada ya michezo 30, ikifuatiwa na Real Madrid wenye pointi 69, huku Villarreal wakishika nafasi ya tatu na pointi 58, na Atletico Madrid wakibaki nafasi ya nne na pointi 57.
Matokeo haya yanaifanya Barcelona kuendelea kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wao, huku mbio za La Liga zikizidi kupamba moto kuelekea mwisho wa msimu.
FT: Atletico Madrid 1-2 Barcelona
⚽ 39’ Simeone
🟥 45+7’ Gonzalez
⚽ 42’ Rashford
⚽ 87’ Lewandowski
FT: Mallorca 2-1 Real Madrid
⚽ 41’ Morlanes
⚽ 90+1’ Muriqi
⚽ 88’ Militao
MSIMAMO: #Laliga
1. Barcelona — pointi 76 (mechi 30)
2. Real Madrid — pointi 69 (mechi 30)
3. Villarreal — pointi 58 (mechi 29)
4. Atletico — pointi 57 (mechi 30)