>

MASTAA SIMBA WAPIGISHWA TIZI KWENYE JUA KALI KINOMA

PABLO Franco, Kocha Mkuu wa Simba  Ijumaa aliwafanyisha mazoezi wachezaji wake mchana wa jua kali ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) dhidi ya Dar City unaotarajiwa kuchezwa leo Jumapili, Uwanja wa Mkapa.

Kocha huyo sambamba na msaidizi wake, Selemani Matola waliwafanyisha mazoezi hayo mida ya saa nane mchana mastaa hao ambapo mazoezi hayo yalifanyika Uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju jijini Dar.

Miongoni mwa mastaa waliokuwa katika mazoezi hayo ni Chris Mugalu, Pascal Wawa, Gadiel Michael, Kenedy Juma, Yusuph Mhilu, Erasto Nyoni, Meddie Kagere, Hassan Dilunga, Aishi Manula, John Bocco na Pape Sakho.

Kwenye mazoezi hayo, Pablo alikuwa akiwasisitiza wachezaji wake hasa safu ya ushambuliaji kuwa makini katika kutumia nafasi ambazo wanazipata. Mabao aliyokuwa akisaka Pablo ilikuwa ni kupitia pembeni kwa Gadiel ambaye alikuwa na kazi ya kupiga krosi kati.

Bernard Morrison, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Jonas Mkude na Rally Bwalya hawakuwa sehemu ya wachezaji waliohudhuria mazoezi hayo.