Waamuzi wasaidizi wawili Wafungiwa mechi ya Dabi ya Kariakoo ya Machi 1

Klabu ya Simba imetozwa faini ya shilingi mil 5 kwa kosa la kuingia uwanja wa Amaan kwa mlango usio rasmi, Faini nyingine ya mil 5 kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kuvalia.

Matukio hayo Yametokea katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo uliochezwa Machi 1 katika uwanja wa New Amaan Complex na kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Aidha klabu ya Simba imetakiwa kulipa gharama za kutengeneza mlango wa chumba cha mkutano wa wanahabari

Waamuzi wasaidizi wawili wamefungiwa kufuatia makosa ya kutafsiri sheria za mpira wa miguu katika mchezo wa Dabi ya kariakoo kati ya Simba na Yanga uliochezwa Visiwani Zanzibar katika uwanja wa New Amaan Complex.

Msaidizi namba moja wa mchezo huo, Kassim Mpanga kutoka Dar es Salaam, amefungiwa miezi sita baada ya kubainika kufanya kosa katika dakika ya 70 kwa kukataa bao halali la Simba akidai kulikuwa na kuotea kabla ya mpira kufungwa. Hata hivyo, tathmini ya wataalamu wa sheria za mpira wa miguu baada ya kuangalia video ya tukio hilo ilionesha kuwa hakukuwa na kuotea, hivyo uamuzi huo ukaonekana kuwa wa makosa.

Aidha, msaidizi namba mbili wa mchezo huo, Hamdan Said kutoka Mtwara, amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria ya kuotea katika dakika ya 61. Katika tukio hilo alionesha kuwa mshambuliaji Prince Dube wa Young Africans alikuwa ameotea, hatua iliyosimamisha shambulizi la timu hiyo dhidi ya Simba.

Baada ya uchunguzi wa video ya tukio hilo kufanywa na wataalamu wa sheria za mpira wa miguu, ilibainika kuwa mshambuliaji huyo hakuwa ameotea wakati mpira unapigwa. Kutokana na makosa hayo, adhabu kwa waamuzi hao imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi Kuu inayohusu udhibiti wa waamuzi.