Simba Yakabiliana na Azam FC Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026

Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inaendelea kutimua vumbi leo Januari 08, 2026 kwa mchezo mmoja wa nusu fainali ya kwanza kati ya Wekundu wa Msimbazi, Simba Sc dhidi ya Azam Fc kwenye Dabi ya Mzizima.

Simba Sc itautumia mchezo huo utakaopigwa katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar majira ya saa 2:15 usiku kujiuliza dhidi ya Wanalambalamba hao baada ya kupokea kichapo cha 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania bara mnamo Desemba 07, 2025.

Ni mechi ya kwanza yenye ladha halisi kwa kocha Steve Barker kwenye kibarua chake kipya ndani ya klabu ya Simba Sc akitarajiwa kukabiliana na mbinu za kocha wa Azam Fc, Florent Ibenge mwenye medali ya ushindi wa kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) 2021-22 wakati akiwa na RS Berkane 🇲🇦.