Arsenal kusitisha mkataba wa udhamini na Visit Rwanda

Arsenal wametangaza kusitisha mkataba wa udhamini wa klabu hiyo wa miaka minane na Visit Rwanda mwishoni mwa msimu wa 2025-26.

Ubia huo ulianza mwaka wa 2018 na mkataba wa sasa unaripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya £10m ($13.3m) kwa mwaka.

Lakini imekuwa chini ya uangalizi baada ya kuongezeka kwa ghasia katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambayo inapakana na Rwanda, ingawa mfumo wa makubaliano ya amani kati ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na serikali ya Congo ulitiwa saini mapema wiki hii.

Mnamo Aprili, Paris St-Germain waliongeza udhamini wao kwa Visit Rwanda hadi 2028, huku Atletico Madrid wakitia saini mkataba wa miaka mitatu wa kubeba nembo hiyo kwenye jezi zao za wanaume na wanawake msimu huu.

Katika taarifa, Arsenal ilisema klabu na bodi ya maendeleo ya Rwanda “wamekubaliana” kumaliza mkataba huo.

The Gunners iliongeza kuwa “imevuka malengo ya awali ya ushirikiano”, ambayo yalikuwa kukuza uhifadhi na utalii endelevu huku pia ikiunga mkono azma ya Rwanda “kuwa kitovu cha kimataifa cha michezo barani Afrika”.

Richard Garlick, afisa mkuu mtendaji wa Arsenal alisema ushirikiano huo umekuwa na jukumu muhimu katika kusaidia The Gunners “kuwekeza katika maono yetu ya muda mrefu ya kushinda mataji makubwa, kwa njia endelevu ya kifedha”.

Mnamo Februari, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilitoa wito kwa Arsenal, PSG na Bayern Munich, ambao pia wanafadhiliwa na Visit Rwanda, kusitisha mikataba inayoghubikwa na “umwagikaji damu” huku kukiwa na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.