
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametangaza mpango wa kujengwa kwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ruvuma–Tunduru hadi Masasi mkoani Mtwara, ili kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo katika mkoa huo.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Boma mjini Masasi leo Jumanne Septemba 23, 2025, Dkt. Samia amesema ujenzi huo utahusisha pia vituo viwili vya kupooza na kusambaza umeme, vitakavyohudumia wananchi na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuandaa mazingira ya ujenzi wa kongani za viwanda wilayani Masasi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi mkoani humo.
Katika hotuba hiyo, Dkt. Samia amezungumzia pia miundombinu ya usafiri, akiahidi kuwa iwapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, serikali itakamilisha ujenzi wa kipande cha barabara ya Mlivata–Mitesa chenye urefu wa kilomita 100, sehemu ya barabara kuu ya Mlivata–Newala–Masasi, kwa kiwango cha lami.
Aidha, ameahidi kuendeleza ujenzi wa barabara za ndani ya mji wa Masasi chini ya usimamizi wa TARURA, ambazo zitajengwa kwa viwango vya changarawe na lami kulingana na mahitaji.