YANGA SC itavuna kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kutokana na kuongeza mahusiano na kampuni ya Haier wakisaini mkataba wa miaka mitatu rasmi Agosti 7 2025 katika Hotel ya Hyatt Regency, Dar.
Rais wa Yanga SC, Injinia Hersi Said amesema kuwa wana matumaini makubwa na mkataba huo kuwa ni faida kwa pande zote mbili kutokana na ukubwa wa Yanga SC na ubora wa bidhaa kutoka Haier.
“Uhusiano wa Haier na Yanga SC ulikuwa na baraka kubwa. Ni matumaini yetu kuwa mkataba huu mpya utakuja na mafanikio zaidi. Msimu wa kwanza na Haier tulifika fainali ya Shirikisho Afrika. Mkataba huu utakuwa wa miaka mitatu mpaka mwaka 2028.
“Uwepo wao kwa mara nyingine unatupa taswira kwamba tutakuwa na matokeo mengine mazuri kwa msimu mpya. Lakini safari hii tumeanza kwanza na ligi yetu ya ndani bado kutakuwa na mazungumzo mengine.
“Nembo za Haier zitakaa mkono wa kushoto kwenye mashindano ya ligi. Mkataba huu utakuwa na thamani ya Tsh bilion 3.3.
“Leo ni moja ya siku ya kihistoria kwa Klabu yetu. Leo tunatangaza kuongeza mahusiano na Haier hii ni taarifa njema sana kwa klabu yetu kwenye uimara wa kiuchumi wa timu yetu.
“Mkataba wa awali ulikuwa mzuri sana. Tulifanya vyema sana kwenye mashindano ya shirikisho ambapo tulifika fainali. Kumbuka hiyo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza tunaingia nao mkataba,”.
Kwa upande wa Ibrahim Kiongozi ambaye ni Meneja wa Kampuni ya Haier Tanzania ameweka wazi kuwa mahusiano ya kampuni hiyo na Yanga SC yameleta mapinduzi makubwa kwenye soko.
“Haier ni kampuni ya vifaa vya kieletroniki vya majumbani kutoka China. Mahusiano ya Haier, Yanga SC na GSM Group na yameleta mapinduzi makubwa.
“Leo tumekuja kutangaza kuwa tunaendelea na mahusiano ambayo yamekuwa na manufaa kwa pande zote tatu.”
Leon Chi Mkurugenzi wa Kanda Afrika Mashariki Haier amesema: “Nimejivunia kuwa sehemu ya watu ambao wamewezesha mahusiano baina ya Haier, GSM na Young Africans SC.
“Nawashukuru sana Yanga SC kwa mchango wao mkubwa kwenye kutangaza bidhaa za Haier na nembo yetu kiujumla. Ni matarajio yetu mahusiano haya yatadumu na kuwa na tija kwa siku zijazo.”
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo na Moyo Wangu Unavuja Damu. Kuvipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371.
Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Msichana wa Maisha Yangu, jiandae kuipata.