DR LIONESS, FOX DIVAZ KUWANIA UBINGWA WA betPawa NBL

 FAINALI ya Wanawake mashindano ya Klabu bingwa ya mpira wa kikapu nchini “betPawa NBL” itafanyika Jumatano Novemba 20, 2024 kwa mechi ya DB Lioness na Fox Divers Uwanja wa Chinangali, mkoani Dodoma.

Fainali hiyo imepangwa kuanza saa 12.00 jioni inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili.

Fox Divaz wamefuzu hatua ya fainali kufuatia ushindi dhidi ya JKT Stars wa 75- 62 wakati DB Lioness imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Vijana Queens kwa 48-44.

Kabla ya mchezo huo wa fainali kutakuwa na michezo miwili. Mchezo wa kwanza utakuwa wa kumsaka mshindi wa tatu kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa kuanzia saa 10.00 jioni kwenye uwanja wa Chinangali A na kufuatiwa na mchezo wa “Classification” kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa kwenye Uwanja wa Chanangali B.

Washindi kwa upande wa wanaume na wanawake watazawadiwa Sh2.8 milioni wakati washindi wa pili watazawadiwa Sh1.4 milioni.

Fedha hizo zimetolewa na wadhamini wakuu, betPawa ambapo zaidi ya Sh144 milioni zimetengwa kwa ajili ya kugharimia gharama mbalimbali pamoja na zawadi.

Washindi wa tatu kwa wanawake na wanaume watazawadiwa Sh700, 000 ambapo wachezaji bora wa mashindano (MVP) kwa wanawake na wanaume kila mmoja atazawadiwa Sh700, 000.

Pia kutakuwa na zawadi ya wafungaji bora, mabeki bora na “best rookie” kwa wanawake na wanaume ambapo watazawadiwa Sh420, 000 kila mmoja na zawadi ya ‘sportsmanship kwa wanawake na wanaume itakuwa Sh280,000.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF), Mwenze Kabinda alisema kuwa wanatarajia ushindani mkali katika michezo hiyo ya mwisho na kwani kila timu imeundwa na wachezaji nyota.

“Si unajua kuwa kila timu inayoshinda, wachezaji 12 na viongozi wanne wanapewa fedha taslimu, Sh140,000 kutoka kwa wadhamini, wakuu, betPawa.

Mpaka sasa, wachezaji wote ambao timu zao zimeshinda wamefaidika na kaisi hicho cha fedha,” alisema Kabinda.

Meneja wa Masoko wa Kanda ya Afrika Mashariki wa betPawa, Borah Ndanyungu alisema kuwa wanajisikia fahari kuwa miongoni mwa wadau wa maendeleo ya michezo nchini hasa mpira wa kikapu.

“Tumeweka bonasi kwa timu ambayo inashinda (Locker Room Bonus) kwa lengo la kuongeza hamasa. Tunashukuru kuona hamasa imekuwa kubwa na ushindani pia,” alisema Borah.

Alisema kuwa wachezaji wameanza kuona tija ya kushiriki katika mchezo huo ambao ni miongoni mwa michezo yenye mashabiki wengi si tu Tanzania, duniani kote.

“Kampuni yetu, betPawa imedhamiria kuleta maendeleo chanya ya mchezo na tunaamini tutafikia lengo hilo.”