>

YANGA: MABAO MENGI YANAKUJA, KUNA MTU ATALIA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa kutokana na mwendo ambao wanakwenda nao ndani ya ligi kuna mtu atalia akiingia kwenye mfumo kutokana na ubora walionao na uwezo wa kutengeneza nafasi.

Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye mchezo wa kwanza wa Yanga uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, Agosti 29 na mwamuzi alikuwa ni William Abel Yanga ilifanya majaribio zaidi ya saba langoni mwa Kagera Sugar.

Shukrani kwa Ramadhan Chalamanda ambaye alianza langoni kikosi cha kwanza aliokoa hatari dakika ya 6, 16, 18, 19, 31, 45, 70 huku mshambuliaji wa Yanga Prince Dube akikosa kufunga nafasi zaidi ya nne ilikuwa dakika ya 2, 18, 21 na 31 hakukomba dakika 90 kwenye mchezo huo.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 25 kwa mguu wake wa kulia akiwa nje ya 18 na Clement Mzize ambaye alianzia benchi na aliingia dakika ya 64 akichukua nafasi ya Dube. Mzize alifunga bao dakika ya 88 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18.

Ally Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanatambua mashabiki wamezoea kuona timu hiyo ikifunga mabao mengi hilo lipo wazi na deni kwa wachezaji kutokana na mwendo wanaokwenda nao kuna timu itafungwa mabao mengi uwanjani.

“Hii iwe kumbukumbu unaona kwamba sasa wanasema hatufungi mabao mengi ni bao moja ama mawili sawa ila wanaangalia nafasi ambazo tunatengeneza na namna ambavyo wachezaji wanaingia kwenye boxi la mpinzani? Kwa namna ambavyo tunakwenda kuna timu itafungwa mabao mengi ikiingia kwenye mfumo.

“Yanga ni timu namba moja kwa kutengeneza nafasi nyingi zaidi ya 20 kwenye mchezo mmoja sasa unadhani ikitokea siku timu ikaingia kwenye mfumo na nafasi zote zikawa ni bao tutafunga mangapi hapo?

Baada ya mechi tatu ambazo ni dakika 270 Yanga imefunga mabao manne na kinara wa utupiaji ni Maxi Nzengeli mwenye mabao mawili aliwafunga Kagera Sugar na KMC.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata 0756 028 371.