YANGA WAPIGA HESABU ZA KIMATAIFA

NAHODHA wa Yanga, Bakari Nondo amesema kuwa makosa ambayo yalitokea kwenye mchezo uliopita ugenini licha ya kupata ushindi yamefanyiwa kazi na benchi la ufundi hivyo wataingia uwanjani wakiwa na hesabu za kupata ushindi kwenye mchezo wao wa kimataifa.

Septemba 21 Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi itakuwa Uwanja wa New Amaan Complex kusaka ushindi dhidi ya CBE SA ya Ethiopia mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 ugenini na mtupiaji akiwa ni Prince Dube.

Nondo alianza kikosi cha kwanza kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa huku Yanga ikitengeneza nafasi nyingi kupitia kwa viungo ikiwa ni Maxi Nzengeli, Aziz Ki, Pacome na kwa upande wa washambuliaji ni Clement Mzize ambaye alitengeneza nafasi dakika ya 86,

Nahodha huyo amesema: “Tulikuwa na kazi kubwa mbele ya wapinzani wetu na tunamshukuru Mungu tulipata ushindi licha ya kutengeneza nafasi kwenye mchezo huo zipo ambazo tulikosa hivyo nina amini benchi la ufundi limeona na litafanyia kazi makosa yaliyopita.

“Kwenye mchezo wetu tukiwa nyumbani hesabu kubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo chanya hilo linawezekana hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Uwanja wa New Amaan Complex.”

Tayari tiketi zinaendelea kuuzwa kwa ajili ya mchezo huo ambao utatoa mshindi atakayetinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click.