KUTOKA Kigoma mwisho wa reli huku wakiwa wanatumia Uwanja wa Lake Tanganyika kwenye mechi za nyumbani, Mashujaa wamewatuliza Coastal Union kwa kusepa na pointi tatu mazima katika mchezo wa ligi wakiwa ugenini.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja ulichezwa Septemba 13 ambapo dakika 15 za mwanzo zilitosha kuwapa ushindi Mashujaa kwa kupachika bao la mapema ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo.
Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC, Mwenge umesoma Coastal Union 0-1 Mashujaa bao likifungwa na Crispin Ngushi dakika ya 14 katika mchezo huo.
Kipa bora msimu wa 2023/24 Ley Matampi atajilaumu mwenyewe alipoamua kutoka kuufuata mpira Ngushi hakukata tamaa mpaka alipomtungua bao hilo kipindi cha kwanza.
Kutoka nafasi ya tano na pointi nne sasa Mashujaa ipo nafasi ya pili ikiwa imekusanya pointi saba kibindoni Simba ni pointi sita nafasi ya tatu na Singida Fountain Gate hawa wapo nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 9 baada ya kucheza mechi tatu wakikomba pointi tatu kwenye mechi tatu mfululizo ambazo ni dakika 270.