TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo Septemba 10inakibarua kingine cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025.
Mchezo wa leo itakuwa dhidi ya Guinea huu ni mchezo muhimu utakaoiweka Stars kwenye nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki michuano ya AFCON 2025 baada ya mchezo uliopita wakiwa Uwanja wa Mkapa kuvuna pointi moja.
Kwenye mchezo uliochezwa Septemba 4 2024 Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Tanzania 0-0 Ethiopia hivyo hakukuwa na timu iliyokomba pointi tatu katika mchezo huo.
Mchezo dhidi ya Guinea utachezwa katika Uwanja wa Charles Konani Benny ambapo wachezaji wa Stars chini ya Kaimu Kocha Mkuu Hemed Morocco wamebainisha kuwa wapo tayari kwa mchezo huo.
Himid Mao amebainisha kuwa wanatambua umuhimu wa mchezo huo na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kusaka ushindi ndani ya dakika 90.
“Wachezaji tupo tayari wapo wachezaji vijana na wenye njaa ya kupambana kwa ajili ya kuona timu inapata matokeo kwa ajili ya taifa hivyo tupo tayari, mashabiki watuombee. Hatuogopi chochote tumekuja kushindana na timu bora itashinda, tupo tayari.”