KOCHA SIMBA: TUNA KAZI KUBWA KUFANYA KUWA IMARA

FADLU Davids, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwa imara kwenye mechi za ushindani ambazo watacheza ndani ya uwanja.

Fadlu mkononi ana tuzo ya kocha bora Agosti 2024 baada ya kuingoza Simba kwenye mechi mbili za ligi ndani ya dakika 180, wakikomba ushindi kwenye mechi zote huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 7 kibindoni ikiwa inaongoza ligi.

Inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki Septemba 7 2024 dhidi ya JKT Tanzania ikiwa ni maandalizi ya mechi za kitaifa na kimataifa ndani ya msimu wa 2024/25.

Kocha huyo amesema kuwa anaamini wachezaji wanajituma kwenye kutimiza majukumu uwanjani kutokana na mazoezi ambayo wanafanya hivyo wana kazi kubwa ya kufanya kutafuta matokeo mazuri kwenye kila mchezo.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya uwanjani kwa kuwa kila mchezo ni muhimu kupata matokeo, ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi lakini tunafurahia kuona kwamba kwenye mechi za mwanzo tumepata matokeo.

“Kuna na matokeo mazuri ni mwanzo wa kujiamini kuelekea mechi zinazofuata kwani kadri unavyopata ushindi hali ya kuhitaji ushindi zaidi inajijenga kwenye akili na mwisho katika utekelezaji uwanjani inakuwa hivyo.”

Mchezo uliopita wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge Simba ilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click.